Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo kupitia viwanda vyake vya sukari vya Mkulazi, Mtibwa Sugar na Kilombero Sugar utazalisha zaidi ya asilimia 70 ya sukari yote hapa nchini hivyo kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo.
Mhe. Malima ameyasema hayo Januari 29, 2024 mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Biashara, Viwanda, Kilimo na Mifugo ambayo imefanya ziara Mkoani humo kujionea hali ya uzalishaji wa sukari pamoja na changamoto zilizopo katika viwanda vya Mkulazi na Mtibwa Sugar.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Mkoa huo utazalisha tani 400,000 kati ya tani 500,000 ambapo kiwanda cha sukari cha Kilombero kitazalisha tani 270,000, Mtibwa Sugar kinatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 100,000 kutoka uzalishaji wa sasa wa tani 70,000 na Mkulazi kitazalisha tani 50,000 hivyo amesema hali hiyo itapunguza hivyo uhaba wa sukari hapa nchini.
“…kwahiyo tani 270000 za Kilombero, tani 100000 za Mtibwa 370000 na tani 50000 za Mkulazi zitakuwa tani 420000 kwahiyo sisi Mkoa wa Morogoro tutakuwa tunazalisha asilimia 70 ya sukari inayohitajika…” amebainisha RC Malima.
Aidha, ametaja mikakati ya mkoa kwa sasa, kuwa ni kuongeza ushiriki wa wakulima wadogo wa zao nilo la miwa ili wachangie uzalishaji wa sukari kwani amesema kwa kufanya hivyo kutainua uchumi wa wakulima wenyewe na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mhe. Malima ametaja sababu zinazochangia upungufu wa uzalishaji wa sukari katika viwanda vilivyopo mkoani humo kwa sasa kuwa ni pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha huku akiwaomba wadau, Bodi ya Sukari pamoja na Serikali kushirikiana kupata suluhisho hasa kwa kipindi hiki ambacho viwanda vimepunguza uzalishaji.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) amempongeza Mkuu wa Mkoa pamoja na watendaji wote kwa kuwa na maono ya kuendeleza sekta ya kilimo cha mazao matano ya kimkakati ambayo ni Karafuu, michikichi, Parachichi, Kakao na Kahawa ambayo yatasaidia kuinua uchumi wa wakazi wa mkoa huo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Biashara, Viwanda, Kilimo na Mifugo Mhe. Deo Mwanyika ameweka wazi lengo la ziara ya Kamati hiyo Mkoani hapo kuwa ni kujionea sababu zinazopelekea uhaba wa sukari kama ambavyo imeelezwa hivi karibuni na Wizara ya Kilimo.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.