Mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni miongoni mwa Mikoa yenye fursa za uwekezaji na rasilimali za kutosha yakiwemo madini ya aina mbalimbali kutokana na mahali Mkoa ulipo na kwamba kinachohitajika ni mipango katika kuendeleza rasilimali hizo na kutumia vema fursa zilizopo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Baraza la Biashara la Mkoa huo lililofanyika Oktoba 9 mwaka huu katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa huo lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kibiashara kwa wakulima, wafanya biashara na wenye viwanda Mkoani humo.
Martine Shigela amesema Mkoa huo kijiografia uko sehemu sahihi kwa wawekezaji, wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda kwa kuwa uko katikati ya miundombinu muhimu ya usafirishaji kama Reli ya Kisasa, Reli ya kati na Reli ya TAZARA huku ikiwa ni kiunganishi cha barabara ziendazo mikoa ya nyanda za juu kusini, mikoa ya kati na ya kaskazini.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa huo umesheheni fursa za kila sekta ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, na kila aina ya madini hivyo jambo pekee ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi ni Wajumbe wa Baraza hilo la Biashara la Mkoa kutambua utajiri huo na kujipanga katika kuendeleza fursa hizo ili kuleta maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa jumla.
“Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ina Big Pontential na sisi tuna pontential kubwa zaidi huenda kuliko maeneo mengine….mtu mwingine anatamani kuwa kwenye mazingira kama haya….” Alibainisha Martine Shigela.
“Kwa hiyo ni eneo ambalo kwa kweli tuone ni fursa kwetu na tulitumie vizuri, lakini pia ina kila aina ya mazao, ina kila aina ya uzalishaji ina kila aina ya fursa, ukisema utalii Morogoro ipo……ukisema madini ndo sisi tuna madini mengi zaidi” alibainisha Shigela.
Katika hatua nyingine, Martine Shigela alilitolea maelekezo suala la wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga waliojengewa vibanda katika Soko Kuu la Chifu Kingalu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro jambo ambalo lililoibuka ndani ya kikao hicho akiwapa wamachinga hao wiki moja kurejea kwenye vibanda walivyojengewa lakini akiwatoa wasiwasi juu ya mikataba wanayoidai kuwa watapewa ifakapo Januari mwakani na kwa muda huu hadi kipindi hicho wataendelea kufanya kazi zao bila kudaiwa chochote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Mwazini Omary Muyanza pamoja na kukiri kuwa kikao cha mwaka huu kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na washiriki wake kutoka sekta mbalimbali kuongezeka, amewashauri wamachinga wa soko la Chifu kingalu kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kurudi maeneo waliyotengewa kwani wanachokihitaji wao ndicho Serikali inakihitaji yaani kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabil Omari Makame alieleza umuhimu wa kikao hicho kuwa sekta binafsi ni Mshirika muhimu katika kuchochea maendeleo ya nchi na ndio maana Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaijali sekta hiyo kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo changamoto ya ulipaji wa ushuru wa huduma.
kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Omari Makame wakimsikiliza mwasilishaji wa mada wakati wa kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele yeye alijikita kuwataka wamachinga wa soko la Chifu Kingalu kwa kumueleza Mwenyekiti wao aliyeshiriki kikao hicho kukaa na wamachinga wenzake kusitisha mara moja zoezi la kuendelea kufanya biashara zao barabarani wakati wamejengewa vibanda vizuri huku akimsishi Mwenyekiti huyo anayesemekana kuwa ndiye kikwazo kikubwa kwa wamachinga kuhamia kwenye vibanda vyao kuachana na ushawishi huo usio na tija.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya akisikiliza hotuba ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya huyo alimueleza mwenyekiti huyo kuelewe kuwa yeye amebeba mustakabali wa maisha ya watu na kuwashawishi wamachinga kutohamia kwenye vibanda walivyojengewa ni matumizi mabaya ya rasilimali fedha zilizotumika kuandaa eneo hilo na zoezi hilo halitaleta picha nzuri kwa viongozi wengi walioshiriki zoezi hilo siku ya uzinduzi wa vibanda hivyo akiwemo Waziri wa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro.
Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Morogoro.
Naye Meneja wa Kongani ya Kilombero inayoshughulikia mpango wa kuratibu kilimo biashara mikoa ya nyanda za juu kusini - SAGCOT Bw.John Mbaga ametaka ushirikiano zaidi baina ya taasisi yake, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Serikali na sekta binafsi ili kufanya kazi kama timu hususan katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo lengo ni kuwasaidia wananchi kulima na kufuga kisasa hivyo kupata matokeo chanya.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria mkutano wa baraza la biashara
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.