MOROGORO NA MKAKATI WA KUREJESHA UOTO WA ASILI.
Mkoa wa Morogoro umejipanga upya kuhakikisha unarejesha Uoto wa asili kupitia Mkakati wa kupanda miti katika Mkoa huo kama sehemu ya kuhifadhi, kutunza, kulinda na kudumisha mazingira ya Misitu na uoto wa asili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akipanda mche wa mti wakati wa Kongamano la wadau wa Mazingira lililofanyika Mei 20 mwaka huu Eneo la Magadu Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Mei 21 Mwaka huu wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Mazingira lililofanyika kwenye ukumbi wa Magadu Mess uliopo Halmashauri Manispaa ya Morogoro, tukio hilo liliambatana na shughuli ya upandaji wa Miti katika Shule ya msingi ya Magadu kama sehemu ya kutekeleza mkakati huo wa kuhifadhi, kulinda na kutunza Mazingira.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni wakati sasa kwa wadau wanaoshughulika na Mazingira kujitathmini na kufanyakazi kwa pamoja kwa kutoa elimu na uwezeshaji wa miche mbalimbali ya miti kwa jamii ili kuhakikisha jamii inawajibika vema katika suala la uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya sasa na ya baadae.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rosalia Rwegasira akipanda mti wakati wa Kongamano hilo.
Aidha, Martine Shigela amesisitiza suala la upandaji miti ili kurejesha hadhi ya Mkoa huo wenye asili ya kuwa na mazingira bora na yenye utulivu kwa binadamu na Wanyama hadi kupelekea uwepo wa mvua nyingi unaosababisha uwepo wa mito mingi inayotiririsha maji yake msimu mzima tofauti na ilivyo sasa.
Mhe. Shigela (wa pili kushoto) akiwa kwenye maandamano na wadau wengine wa mazingira kuelekea eneo la kupanda miti
“Mazingira yetu ndio kila kitu, sote tunakumbukwa kwamba Wasanii waliimba Morogoro maji yanatiririka milimani lakini sasa hivi yanazidi kupungua, sasa lazima kama mkakati wetu ulivyo tuweze kuurudishia hadhi Mkoa wetu wa Morogoro……” amesema Shigela.
“……Kuhakikisha tunahifadhi Uoto wa asili na tunatunza mazingira ili yaweze kututunza na kutusaidia katika Maisha yetu” ameongeza Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameagiza Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wa Serikali Mkoani humo kuhakikisha kila shule inakuwa na vitalu vya miti na kila mwanafunzi kukabidhiwa mche wa mti wa kupanda kila inapofika mwezi Januari ili kuwa na uhakika wa takwimu zinazotolewa za upandaji miti ziwe na uhalisia.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiongea na wadau wa mazingira siku ya Kongamano la Mazingira Mkoani humo Mei 20 mwaka huu
Naye, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amebainisha kwamba Kongamano hilo liwe chachu ya kuubadilisha Mkoa wa Morogoro kwa kuonesha uhalisia wa kupanda miti Mkoa mzima ili kudhihirisha kwa vitendo falsafa ya Morogoro ya kijani.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga(katikati) naye alishiriki kongamano la wadau wa mazingira
Akiwakilisha Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Omary Makame ameweka wazi kuwa ni vema kama Mkoa na Taifa, ajenda ya Upandaji wa Miti na Utunzaji wa Mazingira iwe ajenda namba moja kwani utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni faida kwa kizazi cha sasa na cha baadae.
Wakuu wa Wilaya za Malinyi, Gairo na Morogoro walikuwepo kwenye Kongamano la wadau wa Mazingira na kutoa michango yao namna ya kuhifadhi Mazingira. kutoka kushoto ni Mathayo Maselle Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Jabiri Omary Makame Mkuu wa Wilaya ya Gairo na Alberty Msando Mkuu wa Wilaya ya Morogoro
Kwa upande wake Bi. Saada Shabibi mdau wa Mazingira Kutoka Rukwa ambaye alishiriki Kongamano hilo ameishauri Serikali kuwa, ili kuhakikisha malengo ya utunzaji na uhifadhi wa Mazingira yanafikiwa kikamilifu ni vema Wizara na idara zote za Serikali kufanya kazi kwa pamoja ikiwemo Wizara ya Nishati kupunguza Tozo ya Gesi ili kudhibiti matumizi ya kuni na Mkaa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu Mazingira kwa kukata miti.
Bi. Saada Shabibi (aliyeshika kipaza sauti) akitoa mchango wake wakati wa Kongamano la wadau wa Mazingira.
Aidha Bi. Saada ameishauri Serikali kufanya utafiti wa kupata mbegu za miti zinazokomaa kwa muda mfupi ili kuishawishi jamii kupanda miti hiyo kwa lengo la kuweka uwiano sawa baina ya kasi ya ukataji miti na ukuaji wa miti ili kuziba pengo miti inayokatwa.
Kwenye kongamano hilo pamoja na mada mbalimbali zinazohusu mazingira kutolewa kulienda sambamba na utoaji wa vyeti kwa baadahi ya wadau wa mazingira ishara ya kuwatambua namna wanavyopambana na uhifadhi wa mazingira
Wadau wa Mazingira Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye kongamano
Mhe. Martine Shigela Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (wa tano kulia, waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira Mkoani humo
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.