Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema uongozi wa Mkoa huo unajiandaa kuufanya Mji huo kuwa wa kimichezo zaidi hususan mchezo wa Mpira wa miguu kwa lengo la kushawishi timu mbalimbali za ligi kuja Mkoani humo kufanyia michezo yao.
Mhe. Malima ameyasema hayo Februari 15 mwaka huu mbele ya waandishi wa Habari wakati akizungumza na Mtendaji wa Timu ya KMC ya Manispaa ya Kinondoni Bw. Daniel Mwakasungura Ofisini ikiwa Mkoani humo kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya timu ya Yanga.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha sababu mbalimbali ambazo zimefikiwa kuufanya kuwa Mmkoa wa kimichezo hususan kabumbu kuwa ni Mkoa una vijana wengi wenye vipaji, uwepo wa hali ya hewa nzuri, miundombinu bora ya usafiri kama vile Barabara, Reli ya Kati, Reli ya TAZARA na Reli ya mwendo kasi SGR ambapo zote zinapitia ndani ya Morogoro hivyo wadau wa mchezo kuweza kufika kiurahisi Mkoani humo.
Lakini pia amesema, Morogoro ni mji unaokua kibiashara, uwepo wa vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga za Wanyama, maporomoko ya maji na utalii mwingine uliopo katika milima ya Udzungwa ambapo wanamichezo wanaweza kutembelewa mara baada ya kumaliza mechi zao na kujiliwaza hususan kama timu moja haikupata matokeo mazuri.
Hivyo, Mkoa unaendelea kufanya maboresho ya viwanja vyake ili lengo hilo litimie huku wakilenga pia kutaka kutumia vema mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika Afrika ya Mashaariki 2027.
“...sisi hatumo kwenye viwanja vya AFCON vya kuchezea mechi lakini hatuna sababu ya kutokuwemo kwenye viwanja vya kuchezea mechi za kirafiki na kufanyia mazoezi...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Naye Mtendaji wa timu ya KMC Bw. Daniel Mwakasungura kwa niaba ya uongozi na wachezaji wa timu hiyo amemshukuru Mhe. Adam Kighoma Malima kwa kuikubalia timu hiyo kutumia uwanja wa Jamhuri kwa ajili mchezo wao wa mzunguko wa pili dhidi ya timu ya Yanga.
Timu ya KMC inatashuka dimbani Februari 17, 2024 dhidi ya timu ya Yanga katika uwanja wa Jamhuri Mkoani humo, ambapo KMC inatumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.