Morogoro yajipanga ujenzi vyumba vya madarasa, RC atoa utaratibu mpya.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka Wakurugenzi Watendaji na Madiwani wa Halmashauri zote Mkoani humo kuwa na utaratibu wa kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya wananfunzi wa kidato cha kwanza kila ifikapo mwezi Julai ili kuondokana na mazoea ya kukimbizana na ujenzi huo inapofika mwezi Desemba kila mwaka.
Martine Shigela ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha kujadili namna ya kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kupokelewa mwezi Januari 2022 kilichofanyika katika ukumbi wa CCT uliopo Kilakala katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Baadhi ya Wahe. Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu mara baada ya kikao hicho. wa pili kushoto (waliokaa) ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martine Shigela na wa kwanza kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Mariam Mtunguja
Amesema, viongozi wote wanajua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ambayo hujitokeza kila mwaka lakini bado viongozi hao husubiri maelekezo ya viongozi wa Serikali kutoka juu na ikifika mwezi Disemba kuanza kukimbizana kwa ajili ya kutekeleza maagizo hayo kama vile hawajua uwepo wa changamoto hiyo.
Kwa sababu hiyo, Martine Shigela ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kujipanga katika kukabiliana na upungufu wa madarasa kila ifikapo Mwezi Julai ili ifikapo mwezi Disemba changamoto hiyo iwe imetatuliwa.
‘’.. Kwa nini hatujipangi kuanzia Julai tukaanza kujenga kidogo kidogo kwa nguvu za wananchi na Halmashauri yenyewe, sasa hivi tupo mwezi wa nane tunaingia wa tisa, tuna miezi mitatu ya kujipanga vizuri ili matokeo yakitoka jambo hili liwe limekamilika..” alisisitiza Mhe. Shigela..
Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro Ndg Anza Amen Ndosa akiwa katika picha na Mkuu wa Mkoa huo mara baada ya kikao
Naye Katibu Tawala Msaidizi upande wa Mipango na Uratibu Anza Amen Ndossa amesema, kutokana na upungufu wa madarasa 428, Mkoa unalazimika kuanza mapema kuunganisha nguvu na kuhamasisha wananchi na wadau wengine wa Elimu kujenga vyumba hivyo 428 vya madarasakwa shule za Sekondari kabla ya mwezi Disemba, 2021.
‘’Tusipojipanga mapema baadhi ya wanafunzi watashindwa kujiunga na Kidato cha kwanza kwa kukosa vyumba vya Madarasa’’ Amesema Ndossa.
Mkuu wa Mkoa akiteta jambo na Mtaalamu wake
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajumbe wa kikao hicho wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri na baadhi ya Madiwani pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri, licha ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa kuja na utaratibu wa kuanza maandalizi ya ujenzi wa Vyumba vya madarasa mapema, wamemuahidi kutekeleza maagizo hayo aliyoyatoa ili kuondokana na changamoto hiyo.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga, wa tatu kulia(waliosimama) pamoja na waenyeviti wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro pamoja na madiwani wengine wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa
Baadhi ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro waliohudhuria kikao hicho kama waalikwa
Kwa mujibi wa Katibu Tawala Msaidizi Anza Amen Ndossa, Mkoa wa Morogoro unakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 428 kwa ajili ya wanafunzi 25,300 wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kupokelewa mapema mwezi Januari 2022.
Ni picha ya Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zetu zote tisa za Mkoa wa Morogoro (waliosimama)
Baadhi ya Watendaji wakuu katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya - Makatibu Tawala wa Wilaya - DASs
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho wakiwemo Maafisa Elimu, Mipango, Waweka Hazina na wengine
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi. Joanfaith Kataraia akichangia hoja wakati wa kikao hicho
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.