MOROGORO YAJIPANGA KUKOMESHA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA.
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimetajwa kuongezeka kila kukicha Mkoani Morogoro baada ya kuwepo mfululizo wa matukio ya ubakaji kwa wanawake, Watoto na ulawaiti na kupelekea Mkoa huo kujipanga kudhibiti matukio hayo.
Hayo yamebainishwa Machi 7, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa – RCC kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Magadu Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Malima amesema matukio hayo yameripotiwa kwa kipindi cha Mwezi Februari, 2024 ambapo suala la ubakaji na ulawiti ni miongoni mwa aina ya ukatili ulioripotiwa mara nyingi zaidi huku akibainisha kuwa kwa sasa Mkoa huo umejipanga kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa.
“...ili tuwe mfano kwa Tanzania kwamba hili jambo sisi tumelikasirikia, hatulitaki...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Alex Mukama amethibitisha kuwa matukio ya ulawiti kwa sehemu kubwa yanafanyika shuleni na kwamba jamii imekuwa chanzo cha matukio hayo kutokana na kuziishi baadhi ya mila na desturi zisizofaa.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro Mhe. Christina Ishengoma kwa masikitiko makubwa amesema akinababa kujiingiza kwenye matendo ya ukatili ni jambo baya na ni dhambi kwa mwenyezi Mungu, huku akitaka Elimu zaidi itolewe kwa makundi yote ya akina baba ili kupunguza kasi ya ukatili huo.
Aidha, amewataka wazazi na walimu mashuleni kuchukua nafasi zao kama walezi namba moja katika kufuatilia nyendo vijana/watoto wao na kutaka suala la ukatili liwe ni agenda ya kudumu kwa vikao vyote vya kisheria vinavyofanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Nsemwa amesema ucheleweshaji wa utoaji maamuzi kwa kesi za matukio ya Ukatili kwa baadhi ya taasisi za kutoa haki, kwa sehemu kubwa kunachangia kesi nyingi kutofikishwa Mahakamani na wananchi kuamua kumaliza kesi hizo ngazi ya familia.
Wajumbe wa kikao hicho cha Ushauri kwa Pamoja wamepitisha jumla ya Tsh. 484.054.323,572.61 ikiwa ni Bajeti ya Mkoa huo ya mwaka wa fedha 2024/2025 fedha hizo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na pia kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
Kati ya fedha hizo, fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi 60,340,807,578.00 na fedha za nje ni shilingi 42,853,582,056.00
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.