Kuelekea kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Mkoa wa Morogoro umeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Mkoa huo vinakomeshwa.
Kauli hiyo imetolewa Disemba 7 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akitoa tamko la Mkoa kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akitoa tamko la Mkoa kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ndani ya Mkoa huo.
Katibu Tawala huyo amesema Mkoa wa Morogoro katika kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba 2022 jumla ya matukio 303 yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 347 yaliyoripotiwa katika madawati ya jinsia na watoto ya Polisi kwa kipindi hicho mwaka 2021, matukio yaliyoongoza ni 56 ya ubakaji, 50 ulawiti, 38 mimba kwa wanafunzi.
Aidha, Dkt. Mussa Ali Mussa amesema katika matukio 303 yaliyoripotiwa kwa mwaka 2022, matukio 161 yamefikishwa mahakamani ambapo matukio 35 yametolewa hukumu, matukio 119 yapokatika uchunguzi, 26 yamefungwa, matukio hayo hasa ya kingono yamefanyika kwa kiasi kikubwa kwa wanawake na watoto.
“ Vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto havikubaliki kabisa katika Mkoa wetu, kila mtu ana haki ya kuishi kwa amani na usalama bila kujali kwamba ni mwanamume, mwanamke, motto, mlemavu au asiye na ulemavu...” amesema Dkt. Mussa Ali Mussa.
Sambamba na hilo, Katibu Tawala huyo amesema Mkoa wa Morogoro katika kuadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa mwaka huu 2022, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa kampeni hii katika kila Halmashauri za Mkoa huo, kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia mashuleni, katika mikutano ya hadhara, kwenye nyumba za ibada kupitia viongozi wa dini, makongamano pamoja na vyombo vya habari.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya Abood, TBC na gazeti la Nipashe wakimsikiliza Dkt. Mussa Ali Mussa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro wakati akitoa tamko la Mkoa kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Awali wakati akitoa maelezo ya uelewa juu ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake Bi. Elisia Mtesigwa ambaye ni Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro amesema ukatili ni matumizi ya makusudi ya nguvu au vitisho vinavyofanywa na mtu au kikundi cha watu vinavyoweza kumsababishia mototo madhara ya kimwili, kiafya na kisaikolojia.
Bi. Elisia Mtesigwa akitoa ufafanuzi kuhusu dhana ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake kwenye kikao na waandishi wa habari Mkoani Morogoro.
Aidha, Bi. Elisia amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao na vyombo vyao kupaza sauti ili kuhakikisha kuwa wanatoa elimu katika jamii kutokomeza vitendo vyote vya ukatili katika jamii zao.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Delfina Pacho amesema hata wanaume wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini hawaripoti katika madawati ya jinsia kutokana na kuona aibu hivyo wanaume wameshauriwa kutoa taarifa za unyanyasaji wanaofanyiwa ili kuondoa madhara yatokanayo na ukatili ikiwemo msongo wa mawazo, na kuathirika kisaikolojia, ameongeza kuwa vitaanzishwa vikundi ambavyo lengo lake ni kupaza sauti za wanaume ambao wanafanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mwaka huu ni “ kila uhai una thamani, tokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto” kila mmoja wetu anawajibu wa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa aina zote pamoja na mauaji katika jamii. Maadhimisho hayo yatahitimishwa Disemba 10 mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.