Mkuu wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema Mkoa kupitia sekta ya kilimo umejipanga kufufua mazao ya kimkakati yakiwemo pamba na kahawa ambayo awali yalikuwa yakizalishwa kwa wingi katika Mkoa huo.
Mhe. Malima ameyasema hayo Julai 31 mwaka huu alipotembelea banda la Halmashauri ya Mvomero ikiwa ni maandalizi ya sherehe wakulima na wafugaji Nanenane alitumia fursa hiyo kukagua vipando na mabanda yaliyopo katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya maonesho na sherehe za Nanenane kanda ya mashariki.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema zao la Pamba na Kahawa ni miongoni mwa mazao yenye faida kwa uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla lakini hakuna tija ya uzalishaji wa mazao hayo, hivyo amesema mazao hayo yatawekewa mkazo ili yaendelee kuzalishwa kama awali.
“...kwahiyo hii ni kati ya mazao tunayoenda kuimarisha sana hapa kwetu Morogoro, kahawa kule milimani Mgeta...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa miongoni mwa mazao yatayofufuliwa ni pamoja na kahawa ambapo takribani miche milioni moja ya kahawa itatolewa na Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa (TaCRI) na kupandwa katika Halmashauri za Mvomero na Morogoro.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri kuhamasisha wakulima kulima mazao yenye mchango katika mapato yao, akitolea mfano Halmashauri ya Kilosa imekusanya zaidi ya shilingi milioni 220 kupitia zao la maharage pekee.
Katika ziara hiyo Mhe. Adam Malima aliambatana na Wakuu wa mikoa ya Pwani, Tanga na Dar es Salaam lengo ni kujionea maandalizi ya maonesho ya nanenane ambayo Agosti 1 mwaka huu yatafunguliwa na Mhe. Mizengo Peter Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.