Morogoro yajipanga kwenye kilimo.
Ili wananchi walime kwa tija tunahitaji kufanya mabadiliko ya kifikra katika kilimo na kulima kisasa zaidi ili kuleta tija kwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni Mkoa ulio na rutuba na hali ya hewa nzuri kwa kilimo lakini pia ni Mkoa wenye migogoro mingi ya ardhi kutokana na baadhi ya watendaji kushindwa kusimamia vizuri matumizi ya ardhi.
Hayo yamebainishwa Septemba 28 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Abubakar Mwassa wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa Kilimo lililofanyika Hoteli ya Morena iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuongeza hamasa ya kilimo hususani vijana kutambua kuwa Kilimo ni fursa katika kujipatia kipato na kujiajiri kwa kauli mbiu inayosema “TUNAANZIA SHAMBANI”.
‘‘Licha ya ukubwa Mkoa wa Morogoro wenye ardhi yenye rutuba Mkoa umekuwa haufanyi vizuri katika uzalishaji, mfano zao la mpunga linazalishwa kwa wastani wa tani 2.3 kwa ekari badala tani 6, mahindi tani 1.5 kwa ekari badala ya 6, viazi tani 2.6 badala ya tani 20 na ndizi tani 4.4 badala ya tani 35 na miongoni mwa sababu za uzalishaji huo usio na tija ni kilimo cha kutegemea mvua, matumizi ya mbegu za kienyeji, kutotumia mbolea au mbolea isiyo sahihi, kutokujua hali ya udongo na mazaoyanayostawishwa,,,” Mhe. Fatma Mwassa.
Aidha, ametaja sababu nyingine kuwa ni tabia ya watu kutenga eneo kubwa bila kujali uwezo wa kulihudumia eneo hilo, hivyo kutokana na changamoto ya mvua na uzalishaji usio na tija Mkoa umeamua kuchukua hatua za makusudi kuwa na kongamano ambalo linakwenda kutoa majibu na fursa ya kujifunza, kutathmini na kuamua kwa pamoja nini kifanyike’’.
kongamano hilo litaambatana na tukio la uzinduzi wa msimu wa Kilimo 2022/2023 kimkoa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 3 mwaka huu katika Wilaya ya Kilosa ambapo jumla ya Ekari 5,496 zitagawiwa kwa wakulima ikiwa ni sehemu ya ardhi inayotokana na mashamba tisa (9) ambayo umiliki wake ulibatilishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuona mashamba hayo hayaendelezwi na kwamba sehemu kubwa yatapunguza migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kongamano hilo Prof. Palamagamba Kabudi (MB) amesema uwepo wa kongamano hilo ni fursa nzuri ya utekelezaji wa shughuli za kilimo kwani Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wa unaofaa kwa shughuli za kilimo kutokana na kuwa na ardhi mvua za kutosha na hali ya hewa inayofaa kwa mazao mengi.
Katika hatua nyingine Palamagamba Kabudi amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa msukumo mkubwa aliouweka katika kilimo ikiwemo kuwezesha ujenzi tarajiwa wa skimu mbili kubwa ikiwemo ile ya Kilosa katika kata ya Rudewa.
Azimio kubwa lililojitokeza ndani ya Kongamano hilo ni utuzaji wa vyanzo vya maji na kuthibiti uharibifu wowote wa Mazingira wajumbe wa kikao hicho wakiamini kuwa bila vyanzo vya maji na mazingira mazuri hakuna mvua, hakuna umeme hakuna Kilimo wala ufugaji.
Wadau walioshirikishwa katika kongamano hilo ni pamoja na wabunge, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, wakulima, wauza zana za Kilimo na pembejeo na taasisi za Serikali kama TFS, NEMC, TAWA, TANAPA n.k. lengo kubwa ni kujadili kwa pamoja namna ya kuondoa changamoto za kilimo zinazotokana na mwingiliano wa shughuli zinazofanyika na wadau husika.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.