Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Matrine Shigela amewaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kuitisha vikao vya wadau wa Huduma ya Afya ya Msingi ngazi ya Wilaya ili kujadili kwa kina na kupata njia bora zaidi za kufanikisha zoezi la chanjo ya UVIKO – 19.
Kulia ni amakuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa huo ndugu Doroth Mwamsiku
Martine Shigela ametoa maagizo hayo Aprili 20 mwaka huu wakati wa Kikao cha wadau wa Huduma ya Afya ya Msingi ngazi ya Mkoa (PHC) kilichofanyika Hoteli ya Glonency iliyoko Nanenane katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, pamoja na kuwa chanjo ndani inaendelea kutolewa ndani ya Mkoa bado kasi hairidhishi, kwa sababu hiyo ameagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia vikao vya wadau wa Huduma ya Afya ya Msingi kufsnyika kabla ya Aprili 25 mwaka huu.
“lakini la pili lazima sasa tujipange vizuri tunawezaje kuyafikia haya malengo ngazi ya Wilaya, mkaendeshe vikao vya Afya ya Msingi kwa kila Halmashauri na mipango yetu kwenye mkoa nataka tusivuke tarehe 25 mwezi huu” aliagiza Martine Shigela.
Katika hatua nyingine ameagiza viongozi ngazi ya Wilaya kuwa vikao hivyo vishirikishe wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Dini, watu maarufu, waganga wa tiba mbadala pamoja na machifu lengo likiwa ni kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii nzima kuhusu umuhim wa chanjo ya UVIKO – 19.
“Tuwashirikishe watu maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, Machifu, waganga wa dawa asili wote hao tuwashirikishe kwa sababu mara nyingine watu wetu wanaweza kuamini zaidi viongozi wa hayo makundi” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Remidius Mwema aliyealikwa kushiriki kikao hicho ili kutoa uzoefu wake kutokana na Wilaya yake kuwa miongoni mwa Wilaya zinazofanya vizuri katika utoaji wa chanjo ya UVIKO – 19 amesema viongozi na wahuduma wa Afya ya ngazi ya Jamii wana mchango mkubwa katika zoezi la chanjo na kwa sababu hiyo wanatakiwa kujengewa mazingira mazuri ya utendaji kazi wao na kuwapa ushirikiano wa kutosha.
Aidha, amesema ili kufanikisha zoezi hilo lisionekane ni wajibikaji wa Sekta moj ama kiongozi fulani na wengine kukaa pembeni badala yake zoezi la chanjo ya UVIKO – 19 linatakiwa liwe shirikishi kwa kada zote na viongozi wote kuanzia Mtendaji wa kijiji, Mtendaji wa Kata Afisa Tarafa na wengine na sio kuwaachia wataalamu wa sekta ya Afya pekee.
Kwa upande wao Viongozi wa Dini akiwemo Askofu Jacob Mameo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro amesema Elimu kwa jamii kuhusu umuhim wa chanjo hiyo iendelee kutolewa pasipo kukoma wala kusubiri viongozi wa ngazi ya Mkoa ama Wilaya peka yao.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Ukio Kusirye amesema uzoefu unaonesha kuwa wakati wa Kampeni ya chanjo kunakuwa na mafanikio makubwa ya kuchanja lakini baada ya Kampeni hata kile kiwango cha chini cha malengo husika kinashindwa kufikiwa na kutoa wito kwa kwa kila ngazi ya sekta hiyo kushirikiana ili zoezi la chanjo ya UVIKO – 19 liwe endelevu.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembye akiwasilisha mada katika kikao hicho amesema mpaka sasa Mkoa wa Morogoro una zaidi ya vituo 391 vya kutolea huduma ya chanjo ya Uviko -19 ambapo kila Wilaya kuna zaidi ya vituo 25 mpka 70, lengo likiwa ni kumfikia mlengwa wa chanjo kwa urahisi zaidi badala ya kutumi muda mwingi kutafuta chanjo hiyo.
Kikao cha wadau wa Huduma ya Afya ya Msingi kimefanyika baada ya zoezi la utoaji wa chanjo ya UVIKO – 19 Mkoani Morogoro kuonekana kusuasua na kutofikia malengo yaliyowekwa.
Mkoa huo tangu mwezi Agosti, 2021 zoezi la chanjo lililpoanza mpaka sasa umetoa chanjo ya UVIKO – 19 kwa watu 202, 447 ambao ni sawa na asilimia 15 tu ya lengo tarajiwa la kuchanja watu 1,544,117 wenye umri wa kuanzia miaka 18.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.