Viongozi wa Mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela wamefanya kikao maalum kwa ajili ya kujipanga upya kumalizia ngwe ya pili ya utekelezaji wa zoezi la anwani za Makazi linaloendelea nchi nzima hivi sasa.
Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Morogoro hadi Aprili 12 ndio Mkoa unaoongoza kufanya vizuri katika zoezi la ukusanyaji wa takwimu za anwani za Makazi na kuziweka katika Mfumo wa NAPA na kufikisha asilimia 100.05 ya malengo yake.
Mkoa huo ulijiwekea malengo ya kukusanya takwimu za anwani za Makazi laki sita hata hivyo Pamoja na kuwa halmashauri nyingine hazijakamilisha kazi hiyo bado Mkoa huo mpaka Aprili 12 takwimu zilionekana 618,000 sawa na asilimia 100.05.
Pamoja na mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela ameitisha kikao maalum kwa ajili ya kufanya tathmini ya zoezi hilo na kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya zoezi la uwekaji wa vibao katika Makazi ya watu, taasisi pamoja na vibao elekezi vya Barabara na mitaa.
Martine Shigela pamoja na kuwapongeza viongozi wa Chini yake kwa kufanikisha vema zoezi hilo la ukusanyaji wa takwimuza Anwani za Makazi bado amewataka viongozi hao kuongeza jitihada zaidi kwenye zoezi la uwekaji wa vibao ambalo Kama Mkoa ilikuwa halijaanza kutekelezwa.
Katika kikao hicho ambacho kilihusisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Wajumbe wa Menejimenti ya Mkoa Pamoja na Waratibu wa zoezi la Posti Kodi na anwani za Makazi ngazi ya Wilaya ameelekeza kukamilisha zoezi la uwekaji vibao hivyo kabla au ifikapo Aprili 26 mwaka huu ambapo kila Halmashauri inalazimika kuwa imekamilisha zoezi hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabil Omari Makame kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wenzake amebainisha sili ya mafanikio ya zoezi hilo kwa Mkoa wa Morogoro kuwa ni Maelekezo mazuri ya Mkuu wa Mkoa Martine Shigela, pamoja na Uratibu mnzuri wa Katibu Tawala wa Mkoa huo Mariam Mtunguja kuwa na timu zinazofuatilia zoezi hilo muda wote na kuwa na ushirikiano mkubwa baina ya viongozi wa juu na wa ngazi nyingine.
Nao waratibu wa zoezi hilo ngazi ya Wilaya akiwemo John Mvanga kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara ameshukuru namna Uratibu na ushirikiano mzuri ulikuwepo baina ya ngazi ya kitaifa, Mkoa na waratibu wa Halmashauri.
Amesema, kulikuwa na nafasi na utayari mkubwa kwa ngazi na fursa ya kuuliza swali pale wanapokwama na kusaidiwa. Aidha amebainisha namna wananchi walivyopokea zoezi la anwani za Makazi na kutoa ushirikiano mkubwa kwao.
Mratibu Mvanga amesema uelewa huo kwa wananchi unatokana na uhamasishaji wa kutosha uliokwenda sambamba na utoaji wa Elimu kwao juu ya zoezi hilo hususan faida inayotokana na uwepo wa anwani za Makazi katika jamii.
Kwa sababu hiyo wananchi hata Kama waliendelea kujihusisha na shughuki zao za kawaida ikiwemo kilimo, lakini hawakuondoka kwenda mashambani bila kuacha taarifa zote muhim za zoezi hilo kwa Kiongozi wa mtaa, Kitongoji au kiongozi mwingine wa Serikali suala ambalo anasema liliwarahisishia katika kufanya kazi yao.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.