Imeelezwa kuwa maendeleo ya taifa lolote yanahitaji watu wenye Afya njema na hali bora ya lishe na kwamba hayo yatafikiwa tu iwapo jamii itakuwa na uelewa wa kina juu ya visababisho vya lishe duni katika jamii husika pamoja na njia za kukabiliana navyo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo katika kikao cha tathmini ya Lishe ngazi ya Mkoa kilichofanyika ukumbi wa jengo la NSSF katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akifungua kikao cha tathmini ya Lishe ngazi ya Mkoa
Mhandisi Emmanuel Kalobelo (wa pili kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mdau wa kikao hicho kutoka Benk ya NMB ikiwa ni pongezi kwa kutoa ushirikiano kwao na kutambua kazi nzuri za uratibu wa shughuli za Serikali anazofanya Mkoani humo. wa tatu ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio na wa pili kulia ni mdau kutoka Shirika la Lishe Endelevu Mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya (kushoto) akimsaidia Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kufungua zawadi aliyopewa na wadau.
Akifungua kikao hicho Mhandisi Kalobelo amesema kila eneo la Mkoa huo ni lazima labainishe changamoto zinazosababisha watoto chini ya umri wa miaka mitano kuwa na utapia mlo au udumavu na kukabiliana na changamoto hizo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo amebainisha kuwa lishe duni inachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri Afya ndani ya jamii hususan watoto, akinamama na jamii ya rika zote kwa ujulmla.
‘’Ukikwepa kumpa lishe bora katika umri huu, ukategemea kumpa akiwa mkubwa ni sawasawa na kuupa mmea mbolea wakati umeshakomaa na ushaanza kutoa matunda, tunda litabaki vilevile likisinyaa, tunapaswa kutoa kipaumbele kwa akina mama na wajawazito’’ amesema Kalobelo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo ambaye alikuwa mwenyekiti katika kikao hicho, amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha wanaandaa program za lishe endelevu katika Halmashauri zao kabla au ifikapo Novemba mwaka huu.
Wakichangia mada katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Bi. Siriel Mchembe ameitaka Kamati ya Lishe Endelevu ngazi ya Mkoa kuweka mipango mkakati ya kuwafikia waathirika wa mimba za utotoni hususan wanafunzi ili wafuatilie na kuona Afya zao ili nao waweze kuhudumiwa kama yalivyo makundi mengine katika kupata lishe endelevu.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro Siriel Mchembe akitoa mchango wake wa mawazo namna ambavyo wanaweza kutokomeza lishe duni Mkoani humo hususan kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na wa mimba za utotoni .
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle, ametoa rai kwa Kamati hiyo kutoa Elimu ya lishe kwa Wanaume ili iwasaidie kutambua aina gani ya vyakula wanatakiwa kula na kwa wakati gani, lengo ni kujenga Afya bora ya miili yao na familia kwa ujumla.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira, amewataka wadau mbalimbali pamoja na wataalamu wa Afya kutoa Elimu juu ya ulaji wa vyakula bora kula vyakula vya makundi yote matano badala ya mazoea ya kupenda kula vyakula kwa kufuata radha pekee.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira akichangia mada wakati wa kikao hicho
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Rwegasira ametoa ombi kwa uongozi ngazi za Wilaya, kusimamia maafisa ugani kwenye maeneo yao ili waweze kusimamia mashamba darasa ya mboga za aina mbalimbali ambayo kwayo jamii inaweza kupata Elimu ya kilimo hicho na kujipatia lishe.
Mdau kutoka kituo cha Radio cha United Nation (UN) Ndg. John Kabambala amesema katika kukabiliana na udumavu na Utapia mlo kwa watoto atatoa mchango wake kwa kuandaa vipindi vya Afya vitakavyowasilishwa kwenye vituo vya Afya kupitia TV ili kutoa elimu ya lishe na uzazi wa mpango kwa akinamama wanapokuwa wanasubiri kupata huduma za Afya wawapo katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Kikao hicho cha tathmini ya Lishe kililenga kutathmini hali ya Lishe endelevu ndani ya Mkoa wa Morogoro, hatua zilizochukuliwa na kuweka mikakati ya kuendelea kupambana na lishe duni mkoani humo.
Aidha, kikao kiliwashirikisha wadau ili kusaidia kutatua na kupunguza hali ya udumavu na utapia mlo kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo wadau wengi walitoa ahadi zao ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu ya kupambana na changamoto hiyo kupitia vyombo vya habari.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.