Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema Serikali ya Mkoa huo, kwa kushirikiana na vyombo vya kisheria, imefanikiwa kutatua migogoro lukuki ya wananchi, hususan ya wakulima na wafugaji, ambayo hapo awali ilikuwa changamoto kubwa katika Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa Malima amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Kisheria Duniani Februari 3, 2025 ambapo kwa ngazi ya Mkoa, maadhimisho hayo yamefanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Haki Kanda ya Morogoro, kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema kuwa vyombo vya sheria, hususan Mahakama na taasisi nyingine vimefanya kazi kubwa ya kutenda haki kwa usawa, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa migogoro hiyo.
"Morogoro imepunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji. Awali, Mkoa huu ulitambulika kwa wingi wa migogoro hiyo, lakini sasa hatuna tena," alisema Mhe. Malima.
Aidha, amevitaka vyombo vinavyosimamia haki na usawa kuendelea kushirikiana na Serikali ili kutatua migogoro mingine iliyopo, kwa kufanya hivyo wananchi wataweza kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi kwa manufaa yao binafsi na ya Taifa nzima.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkoa wa Morogoro, Bi. Lightness Tarimo, kwa niaba ya Wakili Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili ya Mkoa wa Morogoro, ameiomba Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania kufanya utafiti wa kina kabla ya sheria kutungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha sheria zinakwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kama inavyolengwa katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Naye, Kaimu Jaji wa Mahakama Kuu ya Morogoro, Bw. Stephen Magoiga, amewasisitiza watumishi wa taasisi za kusimamia haki wanapaswa kufanya kazi kwa uaminifu na kwa weledi wa hali ya juu kwani kukiuka misingi ya uadilifu kunaweza kuongeza migogoro na kuiletea madhara makubwa jamii.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.