Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema Serikali ya Mkoa wa Morogoro imeweka nguvu kubwa katika kuinua sekta ya kilimo hususani kilimo cha viungo kama vile hiriki, karafuu na mdalasini lengo ni kuinua uchumi wa wakulima katika Mkoa huo.
Mhe. Fatma Mwassa ameyasema hayo Januari 24 mwaka huu wakati akipokea miche 10,000 ya karafuu iliyofanyika katika Ofisi za Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) zilizopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema asilimia 85 ya wakazi katika Mkoa huo ni wakulima ambapo wengi wanalima mazao ya chakula lakini hali zao kiuchumi sio nzuri hivyo wao kama Serikali wanajaribu kubuni kilimo ambacho kitapandisha thamani ya maisha yao kwa kuwaongezea kipato.
“...sasa viungo ni miongoni mwa mazao ambayo yanathamani kubwa ukilima hata kama ni kidogo utauza kwa fedha nyingi kwa hiyo tunataka walime sana viungo ili wawe na kipato kikubwa, lengo letu ni kutengeneza wakulima matajiri”. Amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kushawishi kuongeza maeneo mengine kwa ajili ya kuzalisha mazao hayo katika Wilaya za kilombero na ulanga lakini pamoja na faida hizo lengo ni kutunza mazingira katika maeneo hayo.
Sambamba na hilo Mhe. Fatma Mwassa ameomba kupatiwa ushirikiano kutoka kwa taasisi hiyo katika kufanya utafiti wa udongo na hali ya mvua katika Wilaya hizo ili kubaini kama zao la karafuu litaweza kustawi katika maeneo hayo hivyo kuongeza maeneo ambayo zao hilo linazalishwa katika Mkoa huo pamoja na hayo ameipongeza Kampuni ya Viridium kwa kuleta mashine za kuchakata mazao ya viungo kama vile karafuu, tangawizi na hiriki katika Mkoa huo, hivyo kupitia mashine hizo uzalishaji wenye tija utaongezeka Kwa sababu wananchi wengi watahamasika.
Nae Meneja wa kiwanda cha Viridium Tanzania LTD Bwana George Ferreira ambacho kinajihusisha na ukaushaji wa mazao ya viungo kama hiriki na karafuu amesema kiwanda hicho cha kwanza Afrika kina uwezo wa kukausha tani 800 za hiriki kwa mwaka lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa bidhaa hizo za hiriki na uwekezaji walioufanya kwenye kiwanda hicho cha kisasa barani Afrika unagharimu kiasi cha shilingi billion 2, pia amesema wameongeza mashine za kukaushia karafuu ambapo mwishoni mwa wiki hii watakamilisha ufungaji wa mashine hizo katika kiwanda hicho.
Aidha, Meneja Ferreira amesema kuanzia Disemba 16 mwaka 2022 hadi sasa wamenunua tani 100,010 za karafuu kutoka kwa wakulima zenye thamani ya bilioni 1,000,500,000 pamoja na hayo wanatarajia kujenga kiwanda kipya cha kukausha karafuu na kusema kuwa mwishoni mwa mwaka huu ujenzi huo unatarajia kuanza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Kilimo endelevu Bi. Janet Maro ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kwa kuunga mkono juhudi za kuboresha maisha ya wakulima hususani kupitia mazao ya viungo.
Aidha, Bi.Janet amesema kupitia Shirika hilo la kilimo endelevu wameweza kuwafikia wakulima zaidi ya 2,000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambapo takribani miche 200,000 ya karafuu katika Vijiji mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo imepandwa, hata hivyo wapo tayari kutoa ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa mafunzo na miche ili kuhamasisha wananchi kujikita katika Kilimo cha mazao hayo pamoja na kuwashirikisha Maofisa Ugani ili waweze kupata uzoefu wa kilimo hicho.
Taasisi hiyo ya kilimo endelevu kwa kushirikiana na kampuni ya Viridiam imetoa miche 10,000 ambayo imegawanywa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Ulanga, Morogoro Vijijini na Kilombero kwa ajili ya uhamasishaji wa kilimo cha mazao hayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.