Afisa Ustawi wa Jamii Mkoani Morogoro Bi. Jesca Kagunila amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zote za Mkoa huo kushirikiana na Wajumbe wa kamati za watu wenye ulemavu kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya kupiga marufuku vijana wanaowatumia watu wenye ulemavu kupita mitaani wakiomba fedha za kukidhi mahitaji yao.
Bi.Jesca ametoa agizo hilo Novemba 6 Mwaka huu wakati wa kikao cha kujadili huduma zilizotolewa kwa watu wenye ulemavu kwa mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu na kuweka mikakati ya kuunda kamati za watu wenye ulemavu katika Mkoa huo.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika Halmashauri ya Manisapaa ya Morogoro Bi. Jesca amesema haikubariki hata kidogo na ni kinyume cha sheria vijana kuwatumia watu wenye ulemavu kupita mitaani na katika kumbi za starehe kuomba fedha hali inayochangia kuongezeka kwa idadi kubwa ya ombaomba ndani ya Mkoa huo.
Amesema hakuna sababu ya msingi ya kuwepo kwa watu wenye ulemavu kutumika kama vitega uchumi kwa sababu Serikali imetoa mwongozo wa kuwasaidia kwa kila Halmashauri kutenga fedha asilimia mbili zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Amesema, ni vyema watu wenye Ulemavu wakachangamkia fursa hiyo kwa kuunda vikundi ili waweze kupatiwa Mikopo ya Serikali isiyo na riba ili kuendesha maisha yao.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoani Morogoro Bi. Jesca Kagunila (aliyesimama) akiwasilisha taarifa juu ya huduma zilizotolewa kwa watu wenye ulemavu kwa mwezi Julai - Septemba mwaka huu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya watu wenye Ulemavu Mkoa wa Morogoro Bw. Hassan Mikazi amewataka watu wenye ulemavu kutambua utu wao na kukataa kutumika kama kitega uchumi bali wafuate taratibu zinazotolewa na Serikali kwa kujiunga katika vikundi ili wawezeshwe Mikopo.
‘’Ni jambo ambalo linaumiza sana unapokuta kijana mtu mzima barabarani anamkokota mtu mwenye ulemavu wanaomba, ama unamkuta kijana mdogo ambaye umri wake ni wa kwenda shule, hayupo shule anamsindikiza mtu mwenye ulemavu wakaombe’’ amesema Mikazi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya watu wenye Ulemavu Mkoa wa Morogoro Bw. Hassan Mikazi akichangia hoja katika kikao hicho.
Katika hatua nyingine Mikazi ameiomba Serikali kuwachukulia hatua watu wanaowafanyisha watu wenye Ulemavu kazi za ombaomba ili liwe fundisho kwa watu wengine ambao wanatumia fursa hiyo kuwatumikisha watu hao.
Akichangia katika kikao hicho Mjumbe wa Kamati ya watu wenye ulemavu Dkt. Lucy Nkya amesema liandikwe andiko maalum liwasilishwe kwa kamati ya ulinzi na usalama inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ili atoe tamko rasmi kuwachukulia hatu watu watakaobainika wana ombaomba.
Naye, Mwenyekiti wa SHIWAVITA Mkoa wa Morogoro Oskar Changala amebainisha kuwa utafiti ambao ameufanya hivi karibuni umeonesha kuna idadi kubwa ya ombaomba wanaotoka katika Mikoa mingine kuja Mkoani hapa na mara kadhaa amekuwa akiwachukulia hatua lakini bado kuna ongezeko kubwa la watu hao.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya chama cha watu wenye ulemavu Mkoani Morogoro waliohudhuria kikao hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.