Uongozi wa Mkoa wa Morogoro umepokea na kuahidi kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 na kwamba itatekeleza program hiyo kwa kuunganisha na program ya Mapinduzi ya Kilimo cha mazao matano ya kimkakati, lengo ni kuinua maisha ya wananchi kiuchumi.
Hayo yamebainishwa Mei 13 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima wakati akifungua kikao cha kutambulisha Program ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inayojulikana kama Imarisha Uchumi na Mama Samia { IMASA } kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi yake.
Amesema, kwa kuwa utekelezaji wa Sera hiyo unategemea shughuli za kiuchumi za Mkoa husika, Mkoa wa Morogoro utajikita kuhamasisha wananchi katika kupanda mazao matano ya kimkakati ambayo ni Karafuu, Kahawa, Kakao, Parachichi na Michikichi ili kutunza mazingira, kupata kipato cha mazao yenyewe na mwisho kuinua Maisha yao kiuchumi.
“…sasa mimi nataka sisi ajenda yetu Morogoro iwe improving people’s life …nataka tuichukue hii program ya Morogoro tuitumbukize kwenye IMASA…” Amesema RC Adam Malima.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (NEEC) Bibi Being’i Issa akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua kikao hicho amesema, lengo la Programu hiyo ni kutaka kila mwananchi kutekeleza Sera ya uwezeshaji wananchi Kiuchumi kwa kujihusisha kwenye ujasiliamali na kuondokana na dhana potofu ya kila anayefanya biashara ni mhujumu Uchumi.
“…ukiwa mfanyabiashara ulikuwa unaonekana kama ni mhujumu Uchumi, kwa hiyo sasa hivi tulikuwa tunaiondoa hiyo dhana, kuingiza ujasiliamali na watanzania wafanye biashara kila mtu kwa kazi yake…..” amesema Bibi Being’i.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ambaye ndiye msimamizi wa program hiyo, amewataka Watendaji wa Serikali ndani ya Mkoa huo wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutokuwa kikwazo cha utekelezaji wa Programu hiyo,
Aidha, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Elizabeth Mshote amesema maeneo kama Utalii, misitu, madini, nyuki, Sanaa na usafirishaji ni maeneo yanayoakisi Mkoa wa Morogoro yasiachwe kwenye program hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho cha kutambulisha program ya uwezeshaji wananchi Kiuchumi wamekubalina kuwa KILIMO na KUONGEZA THAMANI YA MAZAO YA KILIMO liwe ndilo eneo litakalohusika kuwawezesha wananchi kiuchumi hususan wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.