Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya shikingi milioni 759 kutoka Wizara ya Afya kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD), lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya Mkoani Morogoro.
Akizungumza Januari 17 mwaka huu wakati akipokea vifaa tiba hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake hususan wa Mkoa huo kwani amesema hadi sasa Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa lengo la kuboresha huduma za Afya.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa Mkoa huo umepokea vifaa tiba ambavyo vitasambazwa kwa kila Halmshauri za Mkoa huo ambapo vitagawanywa kwenye zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali huku akisema kuwa vifaa hivyo vitaboresha mara dufu hali ya huduma za Afya kwa wananchi wa Mkoa huo.
“...kwenye Sekta ya Afya tumefanya uwekezaji mkubwa...tunaishukuru sana Serikali na tunamshukuru sana Mhe. Rais...tumemaliza suala la miundombinu kwa kiasi kikubwa sana tunajielekeza kwenye kuboresha kiwango cha ubora wa huduma za afya...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) Kanda ya Mashariki Bi. Betia Kaema amesema Serikali imeendelea kununua dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuboresha huduma za afya hapa nchini ambapo imenunua vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya shilingi bilioni 14.7 ambavyo vitagawanywa nchin nzima.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Morogoro utapatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 759 ambapo kila jimbo litapatiwa vifaa tiba vya shilingi milioni 69 huku na kuongeza kuwa usambazaji huo wa vifaa tiba ni wa awamu ya kwanza vifaa tiba hivyo vitasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Baadhi ya vifaa tiba vilipokelewa Mkoani Morogoro ni pamoja na Vitanda vya wagonjwa 330, vitanda vya kujifungulia mama wajawazito 220, mashuka 1320, magodoro 330 na meza 220 vifaa ambavyo mwakilishi wa Katibu wa Chama cha Mapinduzi - CCM Mkoa wa Morogoro Ndg. Issack Kalleya amewataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinakuwa salama na kutumika kama ilivyokusudiwa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.