Wadau wa maendeleo Mkoani Morogoro wameungana na watanzania wengine kutoa misaada kwa waathirika wa maporomoko ya ardhi katika Mji mdogo wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara.
Hayo yamebainishwa leo Disemba 8, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akipokea msaada wa mkaa mweupe na majiko kutoka Kampuni ya Viridium Tanzania Limited inayozalisha bidhaa hiyo.
Baadhi ya majiko yatakayopelekwa Wilayani Hanang.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 15, Mhe. Adam Malima amesema msaada unaopelekwa Hanang ni tani 10 za mkaa mweupe, majiko 50 na masufuria 500 kwa ajili ya kupikia huku akisema kuwa msaada huo ni wa awamu ya kwanza, msaada wa awamu ya pili kwa wahanga hao ukitarajiwa kupelekwa wiki ijayo.
Huu ni mkaa mweupe ukiwa kwenye mifuko tayari kwa kusafirishwa kwenda Hanang.
"...sisi Morogoro tunapeleka msaada kwa awamu mbili awamu ya kwanza tuna wawahishia mkaa tani 10 na majiko 50..." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza jitihada za kuwapatia msaada wananchi wa Katesh walioathirika na maporomoko hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akipokea Mkaa mweupe na majiko kutoka kwa Afisa Masoko wa Kampuni ya Viridium Tanzania Ltd Bw. Aristotle Nikas kwa ajili ya kupelekwa Hanang.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa Kampuni ya Viridium Tanzania Limited Aristote Nikitas amesema wameamua kutoa mkaa huo mweupe tani 10 na majiko 50 ili kurahisisha upatikanaji wa chakula, pia amesema mkaa huo unahamasisha suala nzima la utunzaji wa mazingira.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM Mkoa wa Morogoro Ndugu Solomon Kasaba amesema chama kinaungana na watanzania wengine kutoa pole kwa waathirika wa maporomoko hayo ya Ardhi yaliyotokea Wilayani Hanang Mkoa Manyara, huku akipongeza juhudi za Serikali kwa kuendelea kutoa misaada kwa waathirika hao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Mkoa wanaendelea na jitihada za kutafuta misaada mingine kwa ajili ya wahanga hao wa maporomoko ya Ardhi kama ambavyo wameshirikiana kupata msaada wa majiko na mkaa mweupe.
Maporomoko hayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 70 huku watu zaidi ya 100 wakijeruhiwa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.