Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania - TAWIRI wakishirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la STEP kufunga vifaa vya kisasa kwa wanyamapori Tembo ili kufuatilia mienendo ya wanyama hao mahali walipo kwa lengo la kutambua maeneo wanayopitia (shoroba) na kurahisisha kufanyika kwa mchakato wa matumizi bora ya Ardhi katika maeneo hayo.
Mathayo Masele ametoa rai hiyo Septemba 3 mwaka huu wakati wa kikao cha uzinduzi wa kamati ya usimamizi wa Ushoroba wa Kilombero wenye urefu wa Km 10 unaounganisha hifadhi ya Udzungwa na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere kilichofanyika katika Hoteli ya Udzungwa Twiga iliyopo katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.
Akiwa Mgeni rasmi katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, Maselle amesema, uwepo wa mitambo hiyo ya kisasa kutambua wanyama wakiwemo Tembo itasaidia kubaini njia wanazopita kwenye makazi ya watu hivyo kuondoa migogoro baina ya Maafisa wa wanyama pori na wananchi wa maeneo yanayopitiwa na shoroba hizo.
‘’Nimefurahishwa na uwepo wa Mkurugenzi Mkuu wa Matumizi Bora ya Ardhi hapa nchini kwani moja ya njia ya kupunguza Adha ya wanyama pori kuingiliana na makazi ya watu ni kufanyika kwa zoezi ambalo ni shirikishi la matumizi bora ya Ardhi yaani kutenga maeneo ya ushoroba’’ amesema Mathayo Maselle.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha baadhi ya majukumu ya kamati ya ushoroba huo kuwa ni pamoja na kusimamia na kurejesha ushoroba, kuhakikisha shughuli za mradi huo zinafanyika kwa ufanisi, kutafuta rasilimali za kuwezesha zoezi hilo linakuwa endelevu pamoja na kusimamia utekelezaji wa miongozo na kanuni za zoezi hilo.
Katika hatua nyingine Mathayo Maselle ametoa wito kwa kamati hiyo kuendelea kuelimisha jamii ili kutambua juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuwaondolea wananchi changamoto ya muingiliano baina ya Makazi ya watu na wanyamapori wanapopita katika ushoroba husika.
Naye Afisa Maliasili Mkoa wa Morogro Bw. Joseph Chuwa, amesema, kwa mujibu wa tathmini zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa kuna mapito ya wanyama (shoroba) 66 hapa nchini ambapo moja ya mapito hayo ni ushoruba wa Kilombero unaounganisha hifadhi ya Milima ya Udzungwa na hifadhi ya Mwalimu Nyerere kupitia hifadhi ya mazingira asilia ya Magombera.
Amesema ujenzi wa ushoroba huo wa Kilombero utasaidia kupunguza vifo vya watu vinavotokana na kuawa na tembo, kuwafukuza tembo hao kwa urahisi na kuongezeka kwa thamani ya Ardhi na ushoroba kuwa sehemu ya utalii hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine, Chuwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali katika nia yake ya kuzifungua shoroba hizo ili kumuondolea mwananchi kero mbalimbali zitokanazo na wanyama pori hususan Tembo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tume ya ushoroba huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bi. Hanji Godigodi amesema kuzinduliwa kwa shoroba hiyo Wilayani kwake, ikiwa ni ya kwanza hapa nchini, imehamasisha Wilaya yake kutakiwa kufanya kazi hiyo kwa ufanisini ili iwe mfano wa kuigwa kwa Mikoa mingine hapa nchini.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dk. Rozaria Rwegasira kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Mariam Mtunguja amepongeza waratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali la mradi wa STEP kwa kuona umuhimu wa kujenga ushoroba katika ukanda wa Kilombelo kwa lengo la kupunguza na kuzuia muingiliano baina ya wanyama na wananchi wa maeneo hayo.
Mkoa wa Morogoro umekuwa Mkoa wa kwanza hapa nchini kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara kuzindua kamati ya usimamizi wa ushoroba wa Kilombero uliopo Wilayani Kilombero.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.