Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoani humo – MORUWASA kuhakikisha wananchi wa kata za Kiegea, Mkundi na Kihonda kupata maji ifikapo Januari 20,2024.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo -Januari 4 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya Maendeleo ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo alitembelea mradi wa ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja lililopo eneo la Kiegea Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Adam Malima amesema, Serikali imeshatoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni moja ambalo litahudumia wakazi wa maeneo ya Kiegea, Star City na Kihonda, hivyo ameitaka MORUWASA kukamilisha maboresho ya mradi huo haraka na ifikiapo Januari 20 mwaka huu mradi huo uwe umekamilika.
“...yeye amesema tarehe 31 tutapata maji sasa mimi namuagiza kwamba tarehe 20 mwezi wa kwanza maji yapatikane...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima ametoa wiki moja kwa MORUWASA kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utaratibu wa kuomba huduma hiyo ya maji ili yaweze kuwafikia ndani ya nyumba zao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA Mhandisi Tamimu Katakweba amesema zoezi la kulaza mabomba kutoka kwenye tanki lenye lita milioni moja limekamilika na wananchi wa maeneo hayo wataanza kufaidi matunda ya Mama Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.