Mpango kabambe wa kuongeza uzalishaji katika Kilimo, Ufugaji na Uvuvi wajadiliwa Morogoro
Mkoa wa Morogoro hivi karibuni umekuwa na kikao kizito cha kuandaa Mpango kabambe wa kuhakikisha Mkoa huo unaongeza uzalishaji katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kupitia kongani ya kilombero lengo ni kuongeza tija kwa wananchi wake na Taifa kwa jumla.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiwa katika kikao cha SAGCOT Machi 15 mwaka huu.
Mkuu swa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiwa kwenye majadiliano wakati wa kikao hicho. kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando
Kikao hicho kilichoshirikisha wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Asasi za Kiraia, Binafsi na Sekta ya Umma Mkoani Morogoro kimefanyika Machi 15 mwaka huu katika Hotel ya Morena iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika kikao hicho kilichoandaliwa na Kongani ya Kilombero inayoshughulikia Kilimo katika Mikoa ya Nyanda za juu kusini mwa Tanzania - SAGCOT kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameweka wazi kuwa Ofisi yake iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya Kilimo ili kuleta tija ya uzalishaji na kuifanya Morogoro kitovu cha Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja akifuatalia kwa karibu mawasilisho yaliyokuwa yakitolewa na wataalam katika kikao cha SAGCOT
Katika kikao hicho wadau hao waliazimia namna ya kutekeleza mpango huo ambapo Sekta ya Umma ikiahidi kuongeza bajeti kwa ajili ya kuimarisha miundombinu vijijini kama vile barabara, nishati ya umeme, usimamizi wa maji na huduma za kijamii ikilenga kuinua uzalishaji katika Kongani ya Kilombero.
Mkurugenzi Mtendaji wa Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT Geoffrey Kirenga amebainisha kuwa Kongani ya Kilombero ilifunguliwa mwaka 2019 hata hivyo haikuanza kazi rasmi kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za miundombinu hafifu ambayo sasa Serikali imeahidi kuongeza bajeti kwa ajili ya kuiimarisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Tanzania Geoffrey Kirenga akieleza malengo ya kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya Morena Mkoani Morogoro
Wadau hao lutoka Sekta ya Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi kwa pamoja walisaini Hati ya makubaliano ya kutekeleza mpango mkakati huo wa kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo, Ufugaji na Uvuvi Hati inayojulikana kama Compact Statement.
Kwa upande wao Sekta Binafsi imeahidi kuazisha majukwaa kwa ajili ya kupashana taarifa za masoko ya mazao na kuhamasisha wananchi ufugaji na uvuvi wa kisasa, kulinda miundombinu ya barabari, pamoja na kuunganisha wakulima, Wafugaji na wavuvi wadogo ili kuwa rahisi kwao kufikika katika kupata mafunzo na mikopo ya kibenki.
Nazo Asasi za kiraia zimeahidi kutoa kwa wakulima mafunzo yanayohusu masuala kifedha pamoja na matumizi bora ya viwatilifu ikiwemo mbolea na mbegu bora za mazao pamoja na kuongeza mahusiano ya karibu baina ya wakulima na wanunuzi wakubwa wa mazao na kutowatumia wanunuzi wa kati wa mazao yao.
Akifunga Kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaagiza Wakuu wa Wilaya, Maafisa kilimo na wataalamu mbalimbali wa Sekta ya Kilimo kushirikiana na Taasisi za tafiti na wataalamu wa Afya ya udongo kufanya tathmini ya kutambua mazao yanayofaa kulimwa katika maeneo yao ili kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.
Aidha, amesema Mkoa wa Morogoro utashirikiana na sekta binafsi na Asasi za kiraia ili kutanua wigo kwa wakulima wadogo, wa kati na wakulima wakubwa ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo, ufugaji na Uvuvi kwa lengo la kukuza kipato chao na kukuza pato la taifa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja akiweka saini hati ya makubaliano ya kukuza uzalishaji wa Cluster ya Kilombero wakati wa kikao kilichofanyika Machi, 15 mwaka huu
”Tutatanua wigo Zaidi ili tuongeze farmers(wakulima) wenyewe tuwasikie kwamba wakulima hawa ambao tunawajua na tunawaona wanahangaika tuwalete hapa wasikie hizi knowledge (maarifa) unauwezo wa kutoka tani 40 au 20 kwa hekta moja hadi kufikia tani 60 au 100 kwa hekta moja” amesema Martine Shigela.
Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya walishiriki kikao hicho. hapa ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wanafunzi wanaomaliza vyuo hapa nchini kujiunga na shughuli za kilimo badala ya kusubiri kuajiriwa serikalini au kwenye makampuni mengine wakati wanaweza kuchangamkia fursa katika Sekta ya Kilimo.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amesema Mkoa huo umejiwekea mkakati kwa kila Halmashauri kujikita kustawisha zao moja mahusus linalostawi katika Wilaya husika ili kuwa na wepesi wa kupatikana kwa wawekezaji na wanunuzi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge mbali na kuipongeza SAGCOT kwa kuandaa kikao hicho amesema Taasisi yake imejipanga kuhakikisha wanazalisha mbegu zenye ubora ili kuleta tija kwenye uzalishaji ndani ya Mkoa huo.
Kongani ya Kilombero ni ya Kongani ya tatu kuanzishwa hapa nchini ikitanguliwa na Kongani ya Mbarali iliyopo Mkoani Mbeya na Kongani ya Ihemi ya Mkoani Iringa ambapo zote zinafikisha 70% ya eneo lote la SAGCOT.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.