Programu za Mradi wa Jifunze Uelewe unaotekelezwa na Shirika la USAID – Jifunze Uelewe Mkoani Morogoro umetajwa kuwa ni chachh ya ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa shule za Msingi Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa Machi 5, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati akizungumza na Wadau wa shirika hilo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Mussa amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa ufaulu unaongezeka lakini pia wadau kupitia miradi yao hususan mradi wa Jifunze Uelewe, umesaidia kwa kiasi kiku wa katika kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule za Msingi.
“... kama Mkoa tumeweza kuyaona matokeo yake kwa sababu hata ufaulu wa wanafunzi kwa miaka hii umepanda kwa kiasi fulani...” amebainisha Katibu Tawala.
Aidha, Katibu Tawala huyo amelipongeza shirika hilo na kulitaka kuendeleza miradi yake ili iwanufaishe wananchi wa Mkoa huo, hata hivyo amesema Ofisi yake ipo tayari kuwasaidia ili kuhakikisha kuwa miardi hiyo inafanikiwa.
Akizungumzia mradi wa Kijana Nahodha, Dkt. Mussa amesema mradi huo unasaidia kuijenga jamii kwani amesema kupitia mradi huo vijana wanajikita kuimarisha miradi yao na kuachana na tabia hatarishi.
Naye Mratibu wa mradi wa Jifunze Uelewe Mkoa wa Bw. Sylvester Isuja amesema wameandaa ziara ya siku ya moja kutembelea shule ya msingi Mwere A iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ili kujionea utekelezaji wa mradi huo katika shule hiyo baada ya walimu wa shule kupatiwa mafunzo na mbinu za ufundishaji.
Kwa upande wake Msimamizi wa miradi ya vijana kutoka Kijana Nahodha Dkt. Tuhuma Tulli amebainisha kuwa mradi wa Kijana Nahodha unawalenga vijana walio katika umri kati ya miaka 15 hadi 25 na kuongeza kuwa mradi huo kwa Mkoa wa Morogoro unatekelezwa katika Halmashauri tatu za Mvomero, Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.