Mrajisi msaidizi wa Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe amewataka Viongozi wa Kijani Amcos Limited wa Gairo kuwa mfano katika uzalishaji wa mazao ya Bustani yakiwemo mboga mboga na matunda ili kukuza chama hicho pamoja na kukuza maendeleo ya Wilaya ya Gairo.
Bw. Shemdoe amesema hayo Juni 4, 2024 wakati akifunga mafunzo elekezi kwa viongozi wa Bodi ya Chama cha Ushirika cha Mazao ya Bustani (Horticulture ) ya Kijani Amcos Limited yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chama cha Walimu Tanzania Mkoani Morogoro .
"... tunataka muwe chama cha mfano kwa sababu Gairo ndio chimbuko la mboga mboga na matunda ili mtu akija anataka kuona Chama cha Bustani tutawaleta kwenu..." Amesema Kenneth Shemdoe
Sambamba na wito huo Bw. Kenneth amewataka Viongozi hao kukamilisha taratibu za kuanzisha stakabadhi ghalani ambapo Chama hicho kitakuwa na nguvu ya pamoja katika kupanga bei ili kuona tija ya mboga na matunda wanayolima.
Sambamba na hilo, Bw. Shemdoe amesema Chama hicho cha Kijani Amcos Limited kimesajiliwa kisheria hivyo viongozi hao wanatakiwa kuendesha Chama kwa Umoja bila kuweka ubinafsi ambao hubomoa zaidi kwani Viongozi hutakiwa kutanguliza maslahi ya wengi kwa tija ya Chama.
Katika hatua nyingine, Mrajisi huyo wa Mkoa amemshuku Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame kwa kuviunga mkono vyama vya ushirika katika kuona fursa za Kilimo biashara Wilayani humo.
Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Wilaya ya Gairo Bw. Omari Issa amewashukuru wataalamu, wawezeshaji pamoja na wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha mafunzo hayo ambayo yatawaongoza Viongozi katika utendaji wa majukumu ya chama kwa maslahi ya wengi na kuahidi kuendelea kusimamia chama hicho ili kutengeneza uhusiano mzuri wa uzalishaji wa mazao ya Bustani.
Kwa niaba ya wanachama, Mwenyekiti wa Chama cha Kijani Amcos Limited Bw.Gabriel Grasiford Balisidya ameushukuru uongozi wa Ushirika na wawezeshaji kutoa mafunzo yatakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao kwani hapo mwanzo hawakujua namna ya utendaji kazi katika chama hicho.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.