Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndugu Amon Mpanju amesema moja ya majukumu ya Wizara hiyo ni kusimamia na kuratibu upatikanaji wa huduma ya Msaada wa Kisheria hapa nchini na jukumu hilo linatokana na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kupanua wigo wa upatikanaji wa haki na kuwafikia wananchi wa pembezoni.
Mpanju amebainisha hayo Julai 6 mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya Kamati ya Uratibu wa Msaada wa Kisheria Mkoa wa Morogoro yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Flomi Mkoani humo.
Amesema, makundi hayo mara kadhaa yamekuwa yakikosa kupata haki zao jambo ambalo ni takwa la kikatiba kwa sababu tu ya hali zao za kiuchumi na kwamba Serikali lazima iondoe hali hiyo kwani kutosaidia upatikanaji wa haki kwa makundi hayo ni kutotekeleza Katiba ipasavyo.
“sasa ili kuwe na usawa lazima ubainishe makundi ambayo hayaifikii huduma hiyo kwa hiyo, ukiangalia suala la huduma ya msaada wa kisheria msingi wake, mzizi wake unatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977”. Amesema Mpanju.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Ndugu Gliffin Mwakapenje yeye alijielekeza kuihimiza Kamati za Uratibu za Mikoa kutumia sheria ya usuluhishi ya mwaka 2020 ambayo ina mifumo inayoruhusu watu waliokinzana kufikia njia ya maridhiano badala ya kupelekena polisi au mahakamani ili kupunguza gharama kwa wahusika wenyewe na Serikali kwani itapunguza pia idadi ya wafungwa magerezani.
Huku Bi. Grace Makwinya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Rasilimali Watu katika Wizara hiyo akieleza majukumu ya Kamati za Uratibu za Mikoa kuwa ni pamoja na kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto, makundi maalum na jamii nzima hususan wale waasio na uwezo katika kutafuta haki zao.
Aidha, Bi Grace amezitaka Kamati hizo kuwa wazi katika utendaji wao wa kazi, kufanya kazi bila upendeleo wala ubaguzi kwa kutumia kigezo chochote kiwe cha hali, jinsia dini au kisiasa.
Nao washiriki wa Kikao hicho wametoa maoni yao namna ya kuimarisha Kamati hizo akiwemo Dkt. Thobias Mnyasenga ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye ametaka kuwepo umakini katika kufanya maridhiano kwa kuwa makosa mengine hayatakiwi kufanyiwa maridhiano ikiwemo ubakaji badala yake makosa kama hayo lazima kuviachia vyombo vya kisheria.
Naye Bi. Marcelina Kibena ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo ya Uratibu wa Msaada wa Kisheria ambaye pia ni kiongozi kwenye shirika la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania – MVIWATA amesema ili Kamati hiyo iweze kufanya kazi yake inavyotakiwa hususan katika kutatua migogoro, ni vema matamko ya wanasiasa hapa nchini yawe yanaendana na mabadiliko ya sheria kwa wakati uliopo.
Kamati za Uratibu ngazi ya Mikoa zimeundwa baada ya kuona kuna umuhimu wa uwepo wa Uratibu wa wadau wanaojishughulisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwenye mikoa huku lengo lake hasa likiwa ni kuwasaidia wananchi kupata haki zao za kimsingi.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.