Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Nawabu Yakubu Almasi (36) aliyekuwa mfanyakazi wa ujenzi katika kiwanda cha sukari Mkulazi amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya kutokea vurugu kati ya Walinzi kutoka Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Magereza (SHIMA) na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari Mkulazi kilichopo Mbigiri Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na wafanyakazi wa ujenzi katika kiwanda cha sukari Mkulazi.
Tukio hilo limetokea Oktoba 17 majira ya saa 12 asubuhi kwenye mlango wa kuningilia kiwandani hapo wakati wafanyakazi hao wakijiandaa kuingia ndani kuanza kazi.
Hawa ni baadhi ya wafanyakazi wa ujenzi katika kiwanda cha sukari Mkulazi
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amefika kiwandani kwa lengo la kutoa pole Kwa tukio hilo na kusikiliza chanzo cha vurugu hizo zilizopelekea kifo cha mtu mmoja. Akitoa majumuisho ya tukio hilo Mkuu wa Mkoa Adam Malima amethibitisha kutokea kwa vurugu kiwandani hapo na kubainisha kuwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na Wilaya pamoja na uongozi wa Kiwanda cha sukari Mkulazi wakitoa pole baada ya kutokea kwa tukio la mauaji.
Aidha, amesema Askari waliohusika na tukio hilo kwa sasa wanashikiriwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali imesikitishwa na tukio lililotokea kiwandani hapi ambalo limepelekea kifo cha mtu mmoja na kuahidi kuwa itasimamia shughuli zote za mazishi.
“...Serikali ya Mkoa inahuzunishwa sana na kifo cha kijana wetu huyu anaitwa Almasi, mimi nimeshaongea na wazazi wake...na Serikali itasimamia mazishi yake kwa kushirikiana na Kampuni ya Mkulazi...kubwa, niseme tu uchunguzi unaendelea...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Hii ni baadhi ya mitambo katika kiwanda cha Sukari Mkulazi
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Mkoa huo kuacha tabia ya kuharibu miundombinu inayojengwa na Serikali Kwa kutumia Fedha nyingi.
Kwa upande wake Mke wa marehem Bi. Shamsa Amir amesema anaamini Serikali itamsaidia kupata haki yake. Ameongeza kuwa mume wake amemuachia watoto wawili wadogo hivyo kifo chake ni pigo kwa familia hiyo.
Bi. Shamsa Amir mke wa marehem Nawabu Almasi
Nao mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Bw. Abdul Salim amesema changamoto kubwa ni suala la ulinzi katika kiwanda hicho ambapo walinzi wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa wafanyakazi na kuwatolea maneno makali ikiwemo kuwatukana.
Bw. Abdul Salim shuhuda wa tukio hilo.
Mwili wa marehem umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku majeruhi wa katika tukio hilo Bw. Said Said amelazwa katika Zahanati ya Kiwanda cha hicho cha sukari na hali yake inaendelea vizuri.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.