Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Zubeir amewataka watanzania kuyalinda mazingira kwa kuwa mazingira ndio uhai wa mwanandamu kwani mazingira ndio chanzo kikubwa cha mvua hapa duniani.
Shekhe Abubakar Zubeir ametoa kauli hiyo Novemba 13 mwaka huu wakati akihutubia waumini wa dini ya kiislam kwenye sherehe ya Mulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) iliyofanyika katika ukumbi wa Tanzanite katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Zubeir akihutubia wananchi kwenye sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika katika ukumbi wa Tanzanite Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Shekhe Zubeir amesema suala la mazingira limetajwa katika kitabu kitukufu cha Kuraan, ambapo Mwenyezi Mungu amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji, utunzaji wa misitu na mazingira yote kwa ujumla.
“...Mazingira yametajwa kwenye Kuraan tukufu,tunzeni mazingira, tunzeni vyanzo vya maji... ” amesema Shekhe Abubakar Zubeir.
Aidha, Mufti amesema kumekuwa na tabia za baadhi ya watu kuharibu vyanzo vya maji, kukata miti hovyo, kuchoma misitu hivyo kutokana na shughuli hizo zimesababisha mvua zisiwe za kutosha katika maeneo mengi hapa nchini.
Sambamba na hilo Shekhe Abubakar Zubeir amewataka wananchi kuendelea kuomba na kuacha maovu ili Mwenyezi Mungu aweze kuleta mvua kwa wakati Pamoja na kuleta neema nyingine kwa watanzania wote.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa salamu za Mkoa, amewataka wakazi wa Mkoa huo kwa Pamoja kutii maagizo yanayotolewa na Viongozi wa Serikali katika ngazi ya Taifa na ngazi nyingine hususan katika suala zima la utunzaji wa mazingira ili kuondokana na uhaba wa mvua unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akisikiliza hotuba kutoka kwa mgeni rasmi Shekhe Abubakar Zubeir kwenye sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Fatma Mwassa amesema kuwa uhaba wa mvua na ukame kwa sasa unatokana na shughuli za kibinadam katika vyanzo vya maji zikiwemo shughuli za uchomaji misitu, kuchungia mifugo kwenye vyanzo vya maji, Pamoja na shughuli za ujenzi maeneo ya milimani, hivyo amewataka wananchi Mkoani humo kulinda mazingira ili kupata mvua za kutosha.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi Mkoani humo kuwapa Watoto wao elimu kwa kuwapeleka shule kwa muda mwafaka ili kuwapa haki ya kupata elimu zote mbili ya duniani na elimu ya dini.
Nae Bw. Fikiri Juma Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Morogoro kwa niaba ya waumini wa dini ya kiislamu katika Mkoa huo ameomba kujengewa Msikiti mkubwa na wa kisasa ili kukabiliana na wingi wa watanzania wanaohamia Morogoro kwa kasi.
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W), Kushoto ni Mhe. Mathayo Massele Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mhe. Jabir Makame Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Ngollo Malenya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Mhe. Albert Msando Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini.
Aidha, Mwenyekiti huo amemsifu Mufti wa Tanzania kwa kuwa mtulivu hivyo kufanya BAKWATA kuwa tulivu tangu aliposhika wadhifa huo.
Hafla hiyo ya Maulid imeenda sambamba na dua ya kumuombea Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uongozi wake ili aweze kuiongoza vizuri nchi yetu kwa matakwa ya mwenyezi Mungu.
Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Zubeir akitoa zawadi za Vitabu vitukufu vya Kuraan kwa Mashekhe wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.