Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zuberi Bin Ally na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima leo Disemba 28, 2024 wameshiriki mazishi ya aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Sheikh Mussa Bolingo aliyefariki Dunia Disemba 27, 2024 saa moja jioni.
Akitoa salamu za msiba huo, Mufti Abubakar Zuberi pamoja na kumshukuru Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugharimia Msiba huo amesema, wamempoteza Kiongozi mahili, mchapakazi na aliyekuwa anafanya kazi yake kwa umahili mkubwa na kuwataka waumini wa Mkoa huo kuwa na Subira.
“nini tunachoweza kusema, tumemkosa mtu, tumemkosa mwanachuoni, tumemkosa mchapakazi na tumemkosa mkombozi wa Mkoa wetu wa Morogoro” amesema Mufti Zuber.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewasisitiza waumini wa dini ya Kiislam kujiendeleza kielimu, elimu dunia na Elimu ya dini yao ili kuwa na maalifa katika kueneza ujumbe wa Mnyazi Mungu.
Aidha, naye ameungana na Mufti wa Tanzania kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushiriki kikamilifu kuwezesha na kufanikisha maziko ya Kadhi Mussa Bolingo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala ambaye katika salam zake za pole aliwataka waumini wa Kiislam na wote walioshiriki mazishi hayo kuenzi mema ya Kadhi huyo, alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amegharimia chakula kwa ajili ya waombolezaji, sanda, usafiri na mambo mengine yote muhimu yaliyohitajika katika kufanikisha mazishi ya Kadhi Bolingo.
Pamoja na salamu hizo, Sheikh wa Mkoa wa Morogoro Twaha Kilango amebainisha kuwa Marehemu Mussa Bolingo aliifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na kwamba katika uongozi wake hadi umauti unamkuta hajawahi kupewa malalamiko ya kazi yake ya Ukadhi aliyokuwa anaifanya ndani ya eneo lake la Mkoa wa Morogoro.
Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abdul Azizi Abood akitoa salamu za pole amesema, Kadhi sheikh Mussa Bolingo alikuwa mpenda maendeleo hususan huduma za kijamii ikiwemo Afya na Elimu ambapo ameahidi kutekeleza ahadi aliyokuwa amemwahidi Marehem ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa ahanati aliyokuwa ameianzisha.
Marehemu Sheikh Mussa Bolingo amezikwa Disemba 28, 2024 baada ya swala ya alasiri katika eneo la msikiti wa Luqman uliopo Kihonda kwa Chambo Manispaa ya Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.