Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro imepata msaada wa gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kutoka shirika lisilo la kiserikali Family Federation for World Peace ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ya kuboresha Sekta ya Afya, hivyo kupunguza vifo visivyo vya lazima kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Makabidhiano ya gari hilo la wagonjwa yamefanyika leo Januari 5 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare na kwamba litatumika katika kituo cha Afya cha Manza kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Loata Sanare amekabidhiwa gari hilo na Mwenyekiti Taifa wa Family Federation For World Peace Ndg. Stylos Simbamwene huku akibainisha kuwa Shirikisho lake lilianza kuunga jitihada za Serikali kwa kujenga Zahanati ya Manza iliyopo Wilaya ya Mvomero na sasa wamefikia hatua ya kutoa gari hilo baada ya kuombwa ili kuboresha huduma ya Afya katika Zahanati hiyo inayotegemewa sasa kuwa Kituo cha Afya.
“Kama tunavyoona tumeletewa Hosptali ya Wilaya ya Mvomero, sisi tunazidi kuchangia maeneo madogo madogo ili huduma hiyo iwe bora zaidi, kwa hiyo kama kiongozi wa Family Federation nilipokea ombi la kuchangia gari, leo nimetekeleza” amesema Simbamwene.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare, amesema, Mkoa huo umejipanga vizuri katika kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kuwa Serikali tayari imeshatoa pesa nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya zote za Mkoa huo, hivyo kazi iliyobaki ni kila Kata kuwa na Kituo cha Afya.
Aidha, Sanare amesema gari hilo litasaidia kuwafikisha wagonjwa katika hospitali ya Rufaa kwa muda muafaka pale ambapo wanapewa rufaa ya matibabu katika hospitali zingine hali ambayo itasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa Sanare ametoa onyo kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kutotumia gari kwa shughuli ambazo hazijakusudiwa kutumika na gari hilo. “Sasa mkalitunze, haiwezekani Mhe. Mkurugenzi gari mkapewa mkaendelea kuhudumiwa na mfadhili aliyewapa, ni mali yenu sasa gari hili lisitumike kubeba vitu vya hovyo, wakati mwingine mnabebea vitu vya hovyo tunaona katika vyombo vya habari” amesema Sanare.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Yusuph Mahunja amemuahidi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kusimamia vizuri matumizi ya gari hilo kwa kufanya kazi ambazo zinazohitajika na kwa kutimiza malengo yake ya kuwahudumia wananchi wa Kituo hicho cha Afya na Halmashauri yote kwa jumla.
Family Federation for World Peace yenye Makao yake Makuu nchini Korea na hapa nchini yakiwa Jijini Dar es Salaam ndiyo waliyojenga zahanati ya Manza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na kwa sasa wanaendelea kuiboresha zahanati hiyo kuwa kituo cha Afya.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.