MWENGE WA UHURU 2024 WAWASILI MOROGORO.
Mwenge wa uhuru mwaka 2024 umewasili leo Aprili 2024, Mkoani Morogoro ukitokea Mkoani Tanga tayari kuanza kukimbizwa Mkoani humo kwa siku tisa. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amepokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Batilda Burian.
Akiongea wakati wa makabidhiano ya mwenge yaliyofanyika katika Kata ya Mziha Wilayani Mvomero Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima amesema Ukiwa Mkoani humo Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa Km 1,730, na utapitia jumla ya Miradi 70 yenye thamani ya Tsh Bil. 19.9 ambapo miradi 18 itawekewa mawe ya msingi, 11 itafunguliwa,18 itazinduliwa na miradi 23 itakaguliwa na kuonwa.
Mwenge huo utakimbizwa Wilaya zote saba (7) za Mkoa huo zenye Halmashauri tisa (9) na kuhitimisha mbio hizo Aprili 29 mwaka huu na kukabidhi Mkoa wa Pwani ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro DC.
Hadi mwandishi wa habari akiandika habari hii tayari Mwenge wa uhuru ulikuwa umeanza kukimbizwa Wilaya ya Mvomero na kufungua mradi mmoja wa kituo cha mafuta cha Matemba wenye thamani ya shilingi milioni 360.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2024 ni tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.