Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Ismail Ali Ussi ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushiriki uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 2025 mwaka huu ili kupata viongozi bora watakaowaletea maendeleo.
Ussi ametoa wito huo wakati akitoa ujumbe wa mwenge wa Uhuru kuhusu mapambano dhidi ya malaria katika Soko kuu la Chifu Kingalu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo pia amegusia suala la uchaguzi wa mwaka huu na kuwataka wananchi hao kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
"Niwaombe na kuwasihi wananchi wa mkoa huu wa Morogoro mjitokeze katika kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu ili muweze kutimiza haki zenu kikatiba na kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo" amesema Ussi.
Aidha, akiwa katika soko hilo la Chifu Kingalu amewataka wananchi hao kutunza miundombinu ya soko akisema serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi katika kuboresha mazingira rafiki ya miundombinu ya soko lao kwa sababu hiyo amewataka wafanyabiashara wa soko hilo kutunza na kutumia vyema soko hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu.
Naye mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Morogoro, huku akimuomba Rais akipendezwa aipandishe hadhi Manispaa hiyo kuwa jiji.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.