JESHI LA POLISI MOROGORO KUFANYA MSAKO WA BANGI
Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro limeagizwa kufanya msako wa mara kwa mara na kufichua biashara ya Bangi inayoendeshwa Mkoani humo ili kuhakikisha vijana wa wa Mkoa huo na watanzania wengine hapa nchini wanabaki salama na kujikita suala nzima la maendeleo ya ujenzi wa Taifa lao.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 31, 2022 na mmoja wa Wakimbiza Mwenge wa kitaifa kwa niaba ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Sahili Geraruma wakati akitoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya shule ya Msingi Lupilo Wilayani Ulanga Mkoani Morogoro.
Ili kukomesha tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya hususan bangi Kiongozi huyo ameliagiza jeshi la polisi Mkoani Morogoro ambao ni mmoja wa mikoa yenye changamoto ya wananchi wachache wanaojihusisha na kilimo haramu cha bangi kufanya msako wa mara kwa mara wa biashara hiyo kwenye maeneo ambayo inafanyika.
“mwenge wetu wa uhuru unaagiza vyombo vya dola hususan jeshi la polisi kufanya msako wa mara kwa mara kwenye maeneo niliyoyataja na maeneo mengine yote yanayoendesha kilimo cha bangi ndani ya Mkoa huu wa Morogoro” ameagiza.
Akibainisha zaidi juu ya mapambano ya madawa ya kulevya chini ya kaulimbiu isemayo “tuelimishane juu ya tatizo la dawa za kulevya tuokoe maisha” Kiongozi huyo kwa niaba ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa amesema vijana wanapotumia madawa ya kulevya hupoteza dira, mwelekeo pamoja na ndoto zao hivyo mwenge huo umewataka vijana kuachana kabisa na matumizi ya dawa hizo hususan Bangi.
Aidha, Mkimbiza mwenge huyo amebainisha maeneo ambayo vijana wengi wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya bishara hiyo ya bangi kuwa ni pamoja na fukwe za bahari, kumbi za starehe, nyumba za kaya maskini na majumba yaliyotelekezwa na kuitaka jamii kupinga biashara hiyo kwa maslahi mapana ya jamii ijayo na taifa kwa jumla.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma akiweka jiwe la Msingi Mradi wa Kituo cha Afya cha Iragua Wilayani Ulanga amesema Serikali ina nia njema na watu wake na ndio maana Mhe. Samia Suluhu Hassan anahangaika muda wote kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo yao.
Hata hivyo amesema nia hiyo njema inafifishwa na watendaji wa Serikali wachache na wasio waaminifu kiutendaji na kuchelewesha maendeleo ya wenzao hususan katika suala nzima la usimamiaji wa miradi ya maendeleo, hivyo amechukua fursa hiyo kuwakumbusha watendaji hao kufanya kazi kwa mujibu wa sharia, kanuni, taratibu na kwa mujibu wa taaluma zao na uzalendo.
Ukiwa Wilayani Ulanga Mwenge wa uhuru umepitia miradi sita yenye thamani ya shilingi za kitanzania ......ambayo yote imekubaliwa na Mwenge huo kuendelea na utekelezaji wake, Mwenge wa Uhuru kesho utakamilisha mbio zake Mkoani Morogoro kwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Mlimba Wilayani Kilombero na siku ya Septemba 02 utakabidhiwa Mkoani Iringa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.