Mwenge wa Uhuru 2021 umeanza kukimbizwa Mkoani Morogoro ambapo leo Agosti 4 umeanza kukimbizwa katika Wilaya ya Kilosa na kufanikiwa kutembelea miradi mitano na kupongeza utekelezaji wake huku ikikataa kuweka jiwe la msingi mradi mmoja.
Akiongea mara baada ya kukamilika kusomwa kwa Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ndg. Yohana Kasitila, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa LT Josephine Paul Mwambashi amesema Mwenge wa Uhuru haukuweza kuweka jiwe la msingi mradi huo kutokana na kukosa nyaraka za malipo ya ujenzi wake.
Amesema, mradi huo ambao unagharimu kiasi cha Tsh. 338 Mil. tayari umeshalipa wakandarasi wa mradi huo jumla ya Tsh. 280 lakini hakuna hati zozote za malipo zilizopatikana, hivyo mwenge wa uhuru pamoja na kuwapongeza Viongozi wa Wilaya ya Kilosa kwa kufanya vizuri miradi mingine minne iliyotembelewa na mwenge lakini hautaweka jiwe la msingi katika mradi huo ambao uko katika kituo cha Afya Cha Mikumi.
Aidha, Lt. Josephine Mwambashi ametumia fursa hiyo kutoa angalizo kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo kuwa wazalendo katika kusimamia miradi hiyo kwa Sababu Serikali inatoa fedha hizo kwa ajili ya watanzania kupata huduma muhimu zikiwemo za Afya, maji na barabara.
Wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo wa Uhuru yaliyofanyika katika Kijiji cha Ruaha Mbuyuni Wilayani Kilosa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela alibainisha kuwa Mwenge wa uhuru 2021 ukiwa Mkoani humo utakimbizwa umbali wa km 1,294.45 na kupitia jumla ya miradi 44 yenye Thamani ya zaidi ya Tsh. 9 Bil.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga alitoa taarifa kuwa mwenge wa uhuru utapitia miradi ya maendeleo mitano yenye thamani ya zaidi ya Tsh.2.2Bil. ambapo kati yao mradi mmoja atazinduliwa, mmoja utawekewa jiwe la msingi, miwili itaonwa na mmoja utafunguliwa huku akisema kuwa miradi hiyo iko katika sekta ya Afya, Maji na Elimu.
Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa miradi yote hiyo Serikali kuu imechangia Tsh.1,348,431,600/=, Halmashauri ya Wilaya ya Kikosa kiasi cha Tsh. 470,993,161 na Tsh. 205,295,000 ni mchango kutoka kwa wananchi.
Mwenge wa Uhuru umepokelewa leo ukitokea Mkoa wa Iringa ambapo ulikimbizwa kwa siku tatu katika Wilaya zake za Mufindi, Iringa na Kilolo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.