Mwenge wa Uhuru waanza kukimbizwa Mkoani Morogoro
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 umeanza kukimbizwa Mkoani Morogoro baada ya kukamilisha kukimbizwa Mkoani Dodoma na kupokelewa Mkoani Morogoro huku ukitarajiwa kupitia miradi ipatayo 50 yenye thamani zaidi ya shilingi 13.5 Bil.
Mwenge huo wa Uhuru umepokelewa leo Agosti 24 ukitokea Mkoani Dodoma na utakimbizwa katika Halmashauri tisa (9) zilizopo katika Mkoa huo ambazo zina jumla ya umbali wa Km 2048.
Akiongea muda mfupi baada ya kupokea mwenge huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Fatma Mwassa amesema Mwenge huo utakimbizwa kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 01 mwaka huu na Septemba 02 Mwenge huo utakabidhiwa Mkoa wa Iringa.
Akiainisha Miradi itakayopitiwa na Mwenge huo, Bi. Fatma Mwassa amesema Mwenge huo wa Uhuru wa mwaka huu 2022 wenye kauli mbiu “sense ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: shitriki kuhesabiwa, tuyafikie maendeleo ya taifa utapitia miradi ya maendeleo 12 ya sekta ya Elimu, Sekta ya Afya 9, Maji 9, Barabara miradi 7, na Utawala Bora mradi mmoja.
Miradi mingine itakayopitiwa na Mwenge huo ni Maendeleo ya Jamii/Vijana miradi 9, Sekta binafsi miradi 3 na kufanya jumla ya miradi yote kufikia 50 huku lengo la miradi hiyo ikilenga kutekeleza azma ya utekelezaji wa Mkakati wa kukuza Uchumi na kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA).
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kulipa mara moja fedha za mfuko wa maendeleo ya vijana wanazodaiwa, kabla ya Mwenge huo wa uhuru haujawasili katika halmashauri zao.
Aidha, Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa ameendeleo kuhimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la Sensa ya watu ambalo limeanza Agosti 24 mwaka huu kwa kuwa amesema sense ya watu ndio msingi wa mipango ya maendeleo na zoezi hilo litachukua siku saba kabla ya kufika mwisho tangu lilipoanza jana Agosti 23.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame katika nyakati tofauti wakati wa kukimbiza mwenge wa uhuru Wilayani kwake, ameaahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mwengewa huo katika kukamilisha miradi ya maendeleo iliyopitiwa ili kuwa bora zaidi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.