Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Ndg. Abdallah Shaib Kaim amewapongeza Wananchi wa Kata ya Namgezi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa kujitolea nguvu zao kuazisha ujenzi wa madarasa matano ya shule Shikizi ya Namgezi iliyopo wiliayani humo.
Ndg. Shaib ametoa pongezi hizo Mei 7 mwaka huu wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa vyumba hivyo vitano vya madarasa ya shule ya msingi Namgezi baada ya mwenge wa Uhuru kuanza kukimbizwa Wilayani humo.
“tunatambua mchango wenu hakika, hii ni level ya uelewa mkubwa, mmehamasika na kutoa michango yenu ninyi ni wananchi wazalendo wa Tanzania...hongereni, mwenge wa Uhuru unawapenda...” amesema Ndugu Abdallah Shaib.
Kwa upande Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Namgezi Bw. Halifa Mlesa akisoma taarifa ya ujenzi wa madarasa hayo ya shule amesema ujenzi huo unahusisha vyumba vitano vya madarasa, Ofisi moja na matundu 6 ya choo huku akibainisha kuwa hadi sasa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 77 na kwamba shule hiyo itaondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa kilometa 8.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Ruaha Tarafa ya Ruaha Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge ameonekana kuridhishwa na ujenzi wa kituo hicho kwa ubora wa vifaa vilivyotumika, ufundi na matumizi ya fedha za mradi huo (Value for Money) na kutaka kuendeleza uaminifu huo na kuwataka kukamilisha haraka mradi huo ili utoaji wa huduma zake uanze mara moja.
Nae, Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ruaha, amesema ujenzi wa kituo hicho uliibuliwa na wananchi kuanzia 2019 kwa kuchimba msingi wa jengo la Wagonjwa wa nje (OPD), unaogharimu shilingi milioni 506, ambapo hadi sasa wamepokea zaidi ya shilingi 382 kutoka Halmashauri.
Mwenge huo wa Uhuru umepitia, kuona miradi miwili, kuzindua mradi mmoja, na kuweka mawe ya msingi miradi mitano yote ikiwa na thamani ya shilingi 1.8 Bil.
Mwenge wa uhuru kesho Mei 8 unatarajia kuendelea na mbio zake Wilayani Malinyi Mkoani humo ikiwa ni siku ya tatu tangu Mwenge huo uingie mkoani Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.