MWENYEKITI CCM MOROGORO ATAKA CHAMA KUWEKEZA KWENYE MADINI
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Mhe. Doroth John amekitaka Chama hicho Mkoani humo kukuza uchumi wake kupitia fursa ya madini yanayopatikana katika Mkoa huo na kuazisha miradi mipya ili kukiimarisha zaidi kiuchumi kupitia Sekta hiyo ya Madini.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Mhe. Dorothy John akiongea na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya CCM Mkoa, Machi 2 mwaka huu
Mwenyekiti Doroth ametoa agizo hilo Machi 2 mwaka huu wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro uliofanyika Wilayani Ulanga Mkoani humo.
Amesema, Mkoa wa Morogoro una utajiri mwingi wa madini karibu Wilaya zote ikiwemo Wilaya ya Ulanga ambayo ina utajiri mkubwa wa madini ya Kinywe (Graphite) ambayo yana ubora mkubwa duniani na kwamba chama kinatakiwa kutumia fursa hiyo kuanzisha miradi yake kwa kumiliki vitalu vya uchimbaji madini kwa lengo la kukiimarisha Chama hicho kiuchumi.
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano huo.
“tunahitaji kuleta miradi mipya ya kiuchumi ndani ya Mkoa wetu, miongoni mwa miradi hiyo tuwekeze kwenye madini yaliyopo kwenye Mkoa wa Morogoro, kwa hiyo kila Wilaya itambue fursa iliyopo ndani ya Wilaya ya Ulanga na Wilaya zingine zenye madini ndani ya Mkoa wetu” amesema Mhe. Doroth.
Kiongozi huyo wa chama Mkoa wa Morogoro ameendelea kusisitiza zaidi kwamba umefika wakati sasa chama hicho Pamoja na kujiimarisha kiuchumi lakini pia kinatakiwa kiwe mfano kwenye masuala ya kiuchumi.
“Twende tukaombe vitalu kisheria tuweze kumiliki na sisi migodi hiyo ili CCM yenyewe iweze kuongoza njia, uongozi ni kuongoza njia, usipoongoza hakuna wa kukuongoza” amesisitiza.
Mhe. Elias Mpanda Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro
Mhe. Ngollo Malenya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga
Maeneo ya machimbo ya mgodi wa madini ya Kinywe uliopo Wilayani Ulanga ambapo wajumbe walipata fursa ya kuutembelea, Machi 2, 2022
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amewapongeza viongozi wa chama hicho ngazi ya Wilaya kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ya UVIKO – 19 na kwamba umoja na juhudi hizo walizoonesha zimemjengea heshima na kuonesha moyo wa shukrani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maeneo ya machimbo ya mgodi wa madini ya Kinywe ambapo wajumbe walipata fursa ya kuutembelea
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.