Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro ndg. Doroth Mwamsiku amewataka wananchi wa Mikoa ya Tanga, Morogoro, Dar es salaam na Pwani pamoja na Mikoa jirani hususan wakulima, wafugaji na wavuvi kushiriki Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayotarajia kuanza Agosti 1, 2022 katika viwanja vya J.K Nyerere Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro ndugu Doroth Mwamsiku akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Michael Waluse juu ya kutumia ardhi kidogo kulima mazao mengi kwa wakati mmoja, alipotembelea Banda la Halmashauri hiyo viwanja vya J.k.Nyerere Nanenane Morogoro Julai 28 mwaka huu.
Bi. Doroth Mwamsiku ametoa wito huo Julai 28 mwaka huu alipotembelea mabanda ya Halmashauri mbalimbali za Mikoa hiyo inayounda Kanda ya Mashariki ili kujionea hali ya maandalizi ya Maonesho hayo na kuwatia moyo waandaji wa mabanda hayo.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Morogoro amebainisha kuwa fursa ya Maonesho ya sikukuu ya Nanenane ni fursa muhimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi wote kwa ujumla kwani ni darasa tosha la kujifunza mbinu za kilimo cha kisasa hasa kutumia ardhi ndogo na Maji kidogo lakini kwa tija kubwa.
“Wito kwa vijana, wananwake na hata Kinababa kujitokeza na kuitumia fursa hii muhimu kwa ajili ya kupata elimu ya mbinu za kilimo chenye tija kupitia Maonesho haya ya Nanenane, uchumi wetu utainuka kwa haraka zaidi” amebainisha ndugu Doroth.
Aidha, Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa upo umuhimu mkubwa wa kupata elimu ya kilimo cha kutumia eneo dogo kwani, ni elimu yenye faida kubwa ya kupunguza au kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji iwapo wafugaji watapatiwa elimu hiyo ili kupanda malisho yatakayoweza kutumika kipindi cha ukame kwa ajili ya mifugo yao.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa ameridhishwa na maandalizi ya maonesho hayo, kwani amejionea vipando mbalimbali vilivyopo katika bustani za Mabanda hayo zikionekana ziko Katika hatua ya mavuno na tayari kwa Maonesho na kufundishia wananchi watakaofika katika Maonesho hayo.
Moja ya zao la Uyoga lililopo katika Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Michael Waluse ametoa rai kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kufika bila kukosa katika Maonesho hayo Banda la Manispaa hiyo ili kujipatia elimu mpya ya kilimo ufugaji na uvuvi ambayo ina tija.
Mkuu wa idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Michael Waluse akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa huo Ndg. Doroth Mwamsiku namna ya kufuga samaki kisasa na kwa gharama nafuu.
Naye, John Kimario ambaye ni mwanzilishi wa Kampuni ya Uyoga ya Okoa amesema, katika Maonesho hayo wakulima watapata elimu ya uandaaji wa mashamba kwa ajili ya kilimo cha Uyoga, zao ambalo ni muhimu katika kukuza uchumi na kuleta kipato cha haraka kwa wananchi.
Moja ya vipando vilivyopo katika Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kama sehemu ya Maandalizi ya Maonesho ya Nanenane yanayotarajiwa kuanza Agosti 1 mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.