Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga amekasilishwa na utendaji kazi usioridhisha wa mkandarasi anayejenga Barabara ya Mfunguakinywa iliyopo Manispaa ya Morogoro na kumuagiza mkandarasi huyo kukamilisha kazi hiyo kabla au ifikapo Novemba Mwaka huu.
Mhandisi Masunga ametoa agizo hilo Oktoba 5, 2024 wakati wa ziara yake pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya Mkoa huo iliyolenga kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mwenyekiti huyo amesema, mradi huo utakaogharimu shilingi Mil. 464 ulipashwa kukamilika Oktoba 8, Mwaka huu, hadi sasa haujakamilika na kutakiwa kuomba muda wa nyongeza ili kukamilisha, huku akiagizwa kutotoa kisingizio chochote cha kutokamilisha kazi hiyo ifikapo Novemba 2024, badala yake akabidhi mradi huo kwa wananchi ili waanze kuutumia.
“…umepewa barabara ya kipande cha mita 350, mwaka mzima mimi naona bado kasi yako ni ndogo hairidhishi sasa tukija hapa mwezi Novemba mradi huu uwe umekamilika…” ameagiza Mwenyekiti huyo wa CCM.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Masunga amewapongeza wasimamizi wa ujenzi wa madarasa 8 na matundu 8 ya vyoo vya shule ya sekondari Mkundi Mlimani kwa usimamizi thabiti na kumaliza ujenzi huo kwa wakati na kuwataka Walimu wa shule hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa Barabara ya Mfunguakinywa Mhandisi Mboka Mkwela amesema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 45 na kudokeza kuwa baada ya kukamilika, barabara hiyo itarahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro na watumiaji wengine lakini pia itakuwa njia mbadala ya kutoka mjini kati kwenda stendi ya mabasi ya Msamvu.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.