Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Vianzi Elias Chapakazi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kukamatwa mara moja kwa tuhuma ya kuuza Ardhi ya wananchi kinyume na sheria za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Loata ametoa agizo hilo Januari 12 mwaka huu Ofisini kwake mara baada ya kikao cha pamoja kilichomhusisha Mkuu wa Wilaya Mvomero Albinus Mgonya, Afisa Ardhi, Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wa vijiji na Kata na Wakulima kutoka katika Halmashauri ya hiyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Vianzi (kushoto) Elias Chapakazi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero akishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuuza Ardhi ya wananchi.
Loata Sanare amesema Mwenyekiti wa Kijiji na au Kitongoji haruhusiwi kuuza Ardhi ya eneo lake la utawala bali anaruhusiwa kupokea maombi ya kuuza ardhi na kuyawasilisha katika serikali ya kijiji na Serikali ya kijiji inajadili kisha kupeleka kwenye mkutano mkuu wa kijiji ili ambapo maamuzi ya kukupa au kumnyima mwombaji wa Ardhi hutolewa.
‘’Naombeni fuateni taratibu zote za kisheria, Mwenyekiti wa Kitongoji haruhusiwi kugawa Ardhi, unachoruhusiwa ni kupokea maombi ya wananchi wako wanaotaka Ardhi lakini maombi yanapelekwa kwenye Serikali ya kijiji, serikali ya kijiji inajadili ikiona kuna sehemu ya kupewa inapeleka kwenye Mkutano mkuu wa kijiji, mkutano mkuu wa Kijiji ndiyo wanaopaswa kukupa Ardhi’’ amesisitiza Sanare.
Katika hatua nyingine, Loata Sanare amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Hassan Njama kumbadilishia kituo cha kazi mtendaji wa Kijiji cha Vianzi Magaly Richard na kumpeleka Mtendaji mwingine ambaye atasimamia zoezi la kupokea barua za Malalamiko ya Ardhi alizokuwa anagawa mwenyekiti wa Kijiji cha Vianzi.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero (wa kwanza kushoto) Albinus Mgonya akisikiliza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Loata Sanare dhidi ya hatma ya mgogoro wa Ardhi uliopo katika Wilaya yake.
Pia, Mkuu huyo wa Mkoa amesema amebaini baadhi ya wananchi wa Vijiji vingine vya Halmashauri hiyo wana barua kutoka kwa barozi wa nyumba kumi wa Chama cha Mapinduzi – CCM ambao wamepewa nyaraka za kuuziwa mashamba na balozi wa nyumba hizo jambo ambalo ni kinyume na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Kwa uopande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya amesema eneo ambalo limehusika sana kuuzwa linamilikiwa na mwekezaji Balozi Namfua ambaye anamiliki hekali 2000 kwa shughuli za kilimo.
Mgonya amesema hekali 2000 ni nyingi kumilikiwa na mtu mmoja hivyo ametuma kamati ambayo inashirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuunda hoja ya kumuomba mwekezaji wa eneo hilo kubaki na hekali 1200 huku hekali 800 zinazobaki ziweze kutumiwa na wananchi endapo mamlaka husika itaridhia mapendekezo hayo.
Aidha, Mgonya ameelezea kuwa wamefanya tafiti na kubaini uwepo wa kaya 72 zina makazi katika eneo hilo ambazo zinaendeleza shughuli tofauti za kibinadamu kutokana na kupewa eneo hilo kinyume na taratibu ambapo hekali 800 kati ya 2000 tayari zinatumika na wananchi hao.
Naye, afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Thomas Nhegeji ameeleza mgogoro wa Ardhi ulipo baina ya kijiji cha Kimambila na Wami Luhindo ambao unapelekea vijiji hivyo kushindwa kugawa Ardhi kwa kufuata sheria au wanafuata sheria lakini wanajikuta wamevuka mipaka ambapo Kijiji kingine kinadai kimeingiliwa kwenye mipaka yake.
Nao wananchi wa vijiji hivyo akiwemo Susu Nestory Susu Mkazi wa Kijiji cha Wamiluhindo, amesema Kiongozi wa Kijiji cha Vianzi alikuwa akiuza maeneo kiholela na hadi kupelekea kuuza maeneo ya vijiji vingine, hivyo ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa uamuzi ambao ameuchukua ili liwe funzo kwa viongozi wengine wa aina hiyo.
Mtendaji wa Kata ya Dakawa Haji Luvanga ametaja sababu kubwa kwa baadhi ya viongozi ngazi ya Kijiji kujihusisha katika kuuza Ardhi kuwa ni kutokana na kutokuwa na uelewa wa utaratibu wa kuuza Ardhi katika maeneo yao, pia viongozi kuwa na tamaa ya fedha katika kazi zao.
Luvanga ametoa wito kwa Watendaji wa Vijiji kuwa karibu na wananchi ili kubaini viongozi ambao wanauza Ardhi bila kufuata kanuni, sheria taratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali.
Naye Elias Chapakazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Vianzi ambaye ni mtuhumiwa wa kosa la kuuza Ardhi ya Kijiji amekanusha madai ya yanayomkabili ya kuuza Ardhi hiyo na kwamba hahusiki na tuhuma hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.