Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Bi. Mary Chatanda amewaonya Wanasiasa wanaotumia majanga yatokanayo na mafuriko ya mvua kutumika kama fursa ya kufanya kampeni za kisiasa katika maeneo yao na badala yake amewataka watoe misaada hiyo kama pole kwa waathirika.
Bi. Mary amebainisha hayo aprili 23, Mwaka huu wakati alipotembelea kata ya Lipangalala katika Halmashauri ya Ifakara Mji Wilayani Kilombero kutoa pole na misaada mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko yatokanayo na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Wilayani humo.
Aidha, Bi. Mary amesema kuwa wananchi wanahitaji faraja na misaada katika kipindi hiki kigumu na sio kueneza siasa kupitia misaada hiyo kwani kufanya hayo hayaleti picha nzuri na si uungwana ndani ya Taifa letu.
"...wapo baadhi ya watu sasa wanataka kutumia majanga haya katika masuala ya kisiasa.... hawaji kutoa misaada bali kuja kupiga porojo za Siasa... "amesema Bi. Mary Chatanda.
Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo ametoa pole na misaada mbalimbali ikiwemo nguo za watoto, vitenge, chakula na vyombo vya nyumbani kwa waathirika ili kuunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwafariji wananchi wanaoathiriwa na majanga hayo hapa nchini.
Pia, amesema baada ya mvua nyingi kupungua serikali itatoa mbegu za mazao za muda mfupi hususan maeneo yaliyoathiriwa kwa ajili ya kupunguza tatizo la chakula na kutoa mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kwani Halmashauri zimeshaelekezwa kuweka utaratibu mzuri wa kupata mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wadau mbalimbali wa sekta binafsi na umma kuendelea kutoa misaada Mkoani humo kwani mafuriko yamekuwa yakiukumba Mkoa huo kwa nyakati tofauti tofauti na kuziomba Halmashauri za Ulanga na Malinyi kuwa wavumilivu na wasikivu wakati serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan sikivu ikijiandaa kuwafikia nao kwani Mkoa huo ni mkubwa na mahitaji ni mengi.
Kwa niaba ya wananchi wenzake Bw. Hamis Saidi Konga mkazi wa kata ya Lipangalala, ameishukuru serikali kwa kuwajali kwani mafuriko hayo yameleta athari kubwa kwa makazi yao kama baadhi ya nyumba kubomoka, kuharibika kwa mazao na hata vifo vya watu wawili na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada kwani mahitaji bado yanahitajika kwa kiasi kikubwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.