Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema anafurahishwa na uwepo wa Gymkhana klabu ya mchezo wa golfu Mkoani humo ambayo inawapa nafasi watoto kukuza vipaji vyao vya mchezo wa golfu na kuweza kutimiza ndoto zao kuwa wachezaji wakubwa wa mchezo huo.
Mhe. Malima amesema hayo Juni 8, 2024 wakati wa maandalizi ya mashindano ya Alliance one Morogoro Open Golfu ambayo yanatarajia kufanyia kuanzia Juni 14 hadi 16 mwaka huu katika viwanja ya Gymkhana vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kupitia programu hiyo ya kuinua vipaji vya golfu katika jamii itaenda kuongeza chachu na thamani ya mchezo huo na utainua vipaji vya watoto hao katika jamii mbalimbali mkoani humo na nje ya mkoa.
".... Nafurahishwa sana na hiyo trend ya Gymkhana Morogoro ya kuinua vipaji miongoni mwa watoto mbalimbali kutoka kwenye jamii ambao tunatarajia baadae wawe wachezaji bora Afrika na Dunia kwa ujumla...." Amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, amewahakikishia washiriki wote wa mchezo huo uwepo wa usalama katika mashindano ya "Alliance one Morogoro open 2024" wakati watakapokuwa katika Mkoa huo, pia amewashukuru wadhamini wote waliojitokeza katika kudhamini mashindano hayo na kupelekea kuwa chachu ya kufanikisha malengo yake.
Pia Mhe. Malima amesema ili kuboresha mashindano hayo zaidi kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha na Sekta ya utalii kwa sababu Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi ambapo washiriki kutoka katika sehemu mbalimbali baada ya kushiriki mchezo huo watapata fursa ya kwenda kuangalia vivutio ikiwemo mbuga za wanyama .
Naye Mwenyekiti wa Morogoro Gymkhana Club ambae pia ni Katibu wa Chama cha Golfu Tanzania Bw. Dickson Sika amewataka wanamorogoro na viunga vya jirani kuwapeleka watoto wao kujifunza mchezo wa golfu ambapo watafundishwa bure (Junior training ) pia ameishukuru sana Serikali ya Mkoa katika kufanikisha mashindano hayo yatakayofanyika hivi karibuni.
Kwa upande wake Kiongozi wa Morogoro Gymkhana Club upande wa wanaume Bw. Seif Mcharo amesema hadi sasa wachezaji zaidi ya 80 wamejisajili kwenye mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika ndani ya siku tatu na kuhusisha vilabu vya Tanzania na nje ya Tanzania pia yatahusisha watoto.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.