Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Mohammed Rajab ameagiza kufanyika haraka zoezi la mpango mkakati elekezi wa Jumuiya ya nchi zilizo kusini mwa Afrika - SADC wa mwaka 2020 - 2030 ili kutoa fursa kwa nchi wanachama kuandaa miradi na programu zitakazojumuishwa pamoja kwa lengo la kupewa fedha.
Balozi Fatma ametoa agizo hilo Septemba 15 mwaka huu kwa wajumbe wa Kamati tendaji wa Wizara mbalimbali wakati wa ufunguzi wa warsha ya kitaifa ya uwekaji gharama katika mpango mkakati elekezi wa maendeleo wa kanda ya SADC – Regional Indictive Strategic Development Plan - RISDP kwa mwaka 2020 – 2030 iliyofanyika katika Hotel ya Antique iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, zoezi la uwekaji gharama katika mpango wa utekelezaji wa RISDP ni maelekezo ya baraza la mawaziri wa SADC katika mkutano uliofanyika Agosti 2021 Lilongwe nchini Malawi, ambapo katika mkutano huo nchi wanachama zilielekezwa kutekeleza zoezi la kukamilisha maoni yao katika sekretarieti ya SADC kabla ya Septemba 30 mwaka huu.
‘’ jukumu hili sio jepesi na ni muhimu likachukuliwa kwa uzito wake na likamilike kama lilivyopangwa ili kuendelea kuilinda sifa hiyo ya Tanzania katika SADC’’ amesema Balozi Fatma.
Aidha, Balozi Fatma amesema lengo la mpango huo ni kuimarisha Ushirikiano katika Kanda kwa ajili ya kuharakisha juhudi za kupunguza umaskini na hatimaye kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Balozi Fatma amebainisha maeneo matano muhimu ambayo mpango huu mpya wa SADC umejikita, maeneo hayo kwanza ni eneo linalohusu Amani, usalama na utawala bora, pili ni maendeleo ya viwanda na ushirikiano wa masoko, tatu ni maendeleo ya miundombinu katika kusaidia ushirikiano wa Kikanda.
Maeneo mengine katika mpango huo ni pamoja na maendeleo ya jamii na watu, tano ni kuhusu Jinsia, Vijana, Mazingira na Mabadiliko ya tabianchi na Usimamizi wa hatari ya Maafa na mwisho ni Usimamizi wa kimkakati wa Mpango Mkakati elekezi wa Maendeleo ya Kanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Agnes Kayola amesema warsha hiyo inajumuisha washiriki kutoka Tanzania bara na Zanzibar ambao watakaa pamoja na sekretarieti ya SADC ili kukamilisha zoezi hilo kabla au ifikapo Septemba 30 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Balozi Kayola amesema Wizara ya mambo ya ndani ina wajibu wa kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinashiriki kikamilifu kuweka gharama kwenye mipango ya kila sekta ambayo inatekelezwa na SADC ndani ya kipindi hicho cha 2020 - 2030.
Naye, Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Tumaini Katunzi amesema mpango huo ni shirikishi kwa wanachama wa Jumuiya ya SADC ambao iwapo utatekelezwa utazibadilisha nchi hizo ziweze kufanya kazi kwa pamoja na kukuza rasilimali zilizopo katika nchi hizo.
Maandalizi ya Mpango huo mpya wa SADC unakuja baada ya Mpango wa awali wa Jumuiya hiyo wa mwaka 2015/2020 kumalizika muda wake huku Mpango huu mpya ukitekelezwa kwa kufuata Dira ya SADC ya mwaka 2020/2030
MWISHO.
Nb: Bonyeza link hapa chini kuangalia taarifa hii.
https://www.youtube.com/watch?v=Ag5A_sMPh6I
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.