Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya ameipongeza Serikali Mkoani Morogoro kwa usimamizi vema utekelezaji wa Afua ya Lishe kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kudhibiti udumavu, ukondefu, na ukosefu wa Madini muhimu mwilini kupitia chakula katika jamii.
Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa pongezi hizo Aprili 21 Mwaka huu katika ziara ya kikazi ya siku mbili aliyoifanya Mkoani Morogoro na kutembelea wadau mbalimbali wanaohusika na utekelezaji wa Afua ya lishe ili kujiridhisha namna ya utekelezaji wake, ambapo alitembelea Viwanda vidogo kadhaa vinavyojihusisha na urutubishaji wa virutubisho katika unga wa sembe ambao ni chakula kikuu kwa jamii ya Watanzania walio wengi.
Naibu Mmuya amesema Mkoa wa Morogoro Umepiga hatua kubwa kwani kwa takwimu za Mwaka 2018 ulikuwa nafasi ya 25 kitaifa katika utekelezaji wa Afua za lishe ambapo kwa takwimu za mwaka huu 2022 Mkoa huo umeshika nafasi tano bora Kitaifa katika utekelezaji wa Mradi wa Afua za Lishe.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu huyo amemuagiza Afisa Biashara wa Mkoa huo kuwatembelea wamiliki wa Mashine za unyunyiziaji wa virutubishi katika unga wa sembe ili kujua na kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wamiliki hao katika utendaji kazi wao hususan changamoto za mitaji ya kuendeshea shughuli zake.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Mmuya amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshaagiza kuwepo kwa ushirikiano baina ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi kufanya kazi kama timu katika utekelezaji wa afua za lishe ili kufikia malengo ya mpango wa pili wa utekelezaji wa afua za lishe ulioanza Mwaka huu hadi Mwaka wa 2025, ambao unalenga kutimia kwa lishe bora kwa Watanzania wote kwa asilimia mia moja.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya SANKU inayojihusisha na kuwasaidia wazalishaji wa kati na wa wadogo katika uwekaji wa virutubishi kwenye vyakula Bw. Omary Gwau amesema kazi yao ni kuisaidia Serikali kupambana na udumavu hapa nchini na kwamba hadi sasa wameshazifikia Wilaya 102 na wazalishaji zaidi ya 700, ambapo Mkoa wa Morogoro pekee wazalishaji 115 wamefikiwa na kuufanya Mkoa huo kushika nafasi ya pili Kitaifa nyuma ya Mkoa wa dar es salaam ambao zaidi wa wadau 120 wamefiwa.
Aidha, Mkurugenzi wa huduma ya urutubishaji wa virutubisho kutoka Wizara ya Afya Bw. Celestine Mgoba amesema katika kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora nje ya kurutubisha unga wa sembe, pia wanafanya urutubishaji kwa kuweka virutubishi katika chumvi, ngano na mafuta ya kula inayopelekea kupungua kwa udumavu, kuongeza uzito na ukosefu wa madini muhimu kwa zaidi ya asilimia 1.8 nchini kote.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TBS amesema wana jukumu kubwa la kusimamia uwekaji sahihi wa virutubishi katika bidha husika ili wananchi waweze kupata bidhaa bora na kuwezesha mlo kamili ambao utapelekea upatikanaji wa lishe bora na kuwezesha malengo ya Serikali ya Mpango ya Afua za lishe kufikiwa kikamilifu ifikapo Mwaka 2025.
Akiwakilisha wadau wa utekelezaji wa uwekaji wa virutubisho katika vyakula ikiwemo unga wa mahindi, Bw. Dornath Makata ambaye ni mmiliki wa kampuni ya uzalishaji ya ASANTE MUNGU iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro amebainisha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa program hiyo ambapo amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu kwa walaji na ukosefu wa mitaji kwa watekelezaji wa uwekaji wa virutubishi katika vyakula.
MWISHO.
|
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.