Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (MB) amewataka Waajiri na Wakuu wa Taasisi za umma hapa nchini ambao hawakupeleka watumishi wao kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kutoa maelezo ya sababu zilizowafanya kutowaruhusu watumishi hao kushiriki michezo hiyo.
Mhe. Dkt. Biteko ametoa agizo hilo Septemba 25, Mwaka huu wakati akifungua rasmi mashindano ya SHIMIWI yanayofanyika katika viwanja mbalimbali vya michezo vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Amesema, kama suala hilo halitekelezeki au lina changamoto basi ni vema jambo hilo likaondolewa au likaboreshwa, lakini kwa sasa kwa kuwa tayari serikali ilishatoa ruksa na kufanya makubaliano ya pamoja, jambo hilo sio la hiari tena bali ni lazima.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Doto amemwagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora kutoa maelekezo kwa waajiri na wakuu wa Taasisi wote kuendelea kutenga bajeti ya michezo ya SHIMIWI pamoja na kutoa ruhusa kwa watumishi wao bila kuwa na kisingizio chochote.
“...Kama tumekubaliana kufanya jambo lazima tulifanye, linakuwa ni lazima siyo hiari, Kama kuna sababu ya kuliboresha tuboreshe kwa kufanya mabadiliko na siyo kukubaliana bila kufanya utekelezaji...” ameagiza Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Dkt. Biteko amechukua hatua hiyo kutokana na kushuka kwa idadi ya vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo kutoka 74 mwaka 2023 hadi 66 mwaka 2024 jambo ambalo amesema linaashiria uwepo wa changamoto katika uendeshaji wa michezo ya SHIMIWI.
Sambamba na hayo, Mhe. Doto Biteko amewataka viongozi wa mashindano ya SHIMIWI kuhakikisha mashindano yajayo wanaweka mpango wa kuendeleza vipaji vya watu wenye mahitaji maalum na kuyaboresha zaidi kwa ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amepongeza juhudi za viongozi wa SHIMIWI kwa kutumia muda mchache kuandaa michezo mbalimbali kwa watumishi ili kuwa na afya ya akili na ya mwili hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wawapo ofisini.
Pia amesema, Taifa limekuwa na mwendelezo mzuri katika mashindano ya kimataifa kwani katika timu ya Taifa Stars ina nafasi nzuri kufuzu katika kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani Nchini Moroco.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo unasifika kuwa ni Mkoa wa kimichezo kutokana na Amani iliyopo ambayo ndio chachu ya maendeleo huku akiwahakikishia wanamichezo waliofika mkoani humo kufanya michezo yao kwa utulivu na amani.
Hata hivyo, Mhe. Malima amewataka wanamichezo hao mara baada ya kuhitimisha michezo hiyo watumie fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana Mkoani Morogoro vikiwemo Mbuga ya wanyama ya Mikumi, hifadhi ya Mwalimu Nyerere na milima ya Udzungwa yenye vivutio vya kila aina yakiwemo maporomoko ya maji.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.