Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega amesema amelipokea ombi la kutaka somo la michezo kuwekwa rasmi kwenye mitaala ya masomo ili kuwapa fursa walimu wa michezo hapa nchini kupanga ratiba zao katika kufundisha somo hilobadala ya ilivyo sasa ambapo somo hilo halipo kwenye mitaala hiyo.
Waziri Ulega ametoa Kauli hiyo Januari 28, mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja katika Wilaya za Mvomero na Morogoro Mkoani humo alipotembelea shule teule za michezo ili kujua maendeleo ya michezo na kuona changamoto wanazokabiliana nazo.
Akipokea taarifa za Shule ya Msingi ya Manyinga na shule ya Sekondari ya Lusanga zilizopo katika Tarafa ya Tuliani Wilayani Mvomero ambazo ni shule teule za michezo, Naibu Waziri Ulega aliombwa somo la michezo kuwekwa kwenye mitaala ya Serikali ili walimu wawe huru katika kupangilia masomo yao namna ya kuwafundisha wanafunzi wao.
Waziri Ulega pamoja na kuwapongeza walimu kuendelea kufundisha somo hilo kwa shida kwa sababu ya kutokuwepo kwenye mitaala ,alipokea Ombi hilo na kwamba anakwenda kulishughulikia.
“kwamba hautambui moja kwamoja kipindi cha Michezo, kwa hiyo walimu mnapata tabu sana namna ya kupangilia, hili jambo nimelichukua na sisi serikali tunakwenda kulijadili, kushauriana na wenzetu wa Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI na sisi wa habari kuhakikisha kwamba shughuli za Sanaa, Utamaduni na Michezo zionekane moja kwa moja ili kuwapa nafasi nivyi walimu muweze kuwa huru katika kujipangia mipango yenu ya kiratiba” alisema Waziri Ulega.
Aidha, Waziri Ulega ametoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi, kutodharau kipindi cha michezo kwa kuwa ni muhimu kwa watoto kwa kuwa Michezo ni Sehemu ya Elimu na humjenga mwanafunzi kujiamini katika maisha, hivyo wasikubaliane na watoto wao wanaodharau vipindi vya michezo.
“Msikubaliane na watoto wenu wanaorudi nyumbani na kusema sasa hivi baba kule shuleni hakuna chochote tunacheza tu, mwambie chukua madaftari yako, beba begi lako nenda kacheze huko shuleni mpaka uruhusiwe na mwalimu” Waziri Ulega alisisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri amewataka viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya kuhakikisha wanasimamia viwanja vya michezo mashuleni visibadilishiwe matumizi badala yake vibaki kwa ajili ya matumizi ya michezo, kwa kuwa dunia ya leo michezo ni ajira, michezo ni Uchumi na kupitia viwanja hivyo ndivyo tutawapatia vijana wetu ajira na kukuza uchumi wao na wa Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albino Mgonya, akimkaribisha mgeni wake, amesema Serikali ngazi ya Wilaya hiyo, inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi - CCM katika kuhamasisha na kuimarisha virabu mbalimbali vya michezo kama inavyoelekezwa kwenye ilani ya chama hicho Ibara ya 242.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Mvomero ameiomba Serikali, pamoja na kufanya vizuri katika kutilia mkazo suala ya michezo, kuendelea kutupia jicho la pekee kwenye shule teule za michezo kuwa na walimu wa michezo wa kutosha ili kutekeleza azma ya Serikali katika kuibua vipaji mbalimbali miongoni mwa vijana.
Walimu wa shule alizotembelea Naibu Waziri Ulega kwa nyakati tofauti wameeleza changamoto zinazowakabili. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Lusanga Bahati Omari amesema changamoto wanayokabiliana nayo kukosekana kwa mfumo rasmi wa kuendeleza vipaji vya wanafunzi unaotokana na kukosekana kwa muunganiko wa somo la Elimu ya Michezo au Elimu ya Viungo (Physical Education – PE).
Amesema muunganiko huo unakosekana baina ya madarasa ya chini yaani kwa shule ya msingi na “O” level ambako somo hilo lipo na Elimu ya Sekondari “A” level ambako somo hilo halipo, hivyo kutokuwa na Taasusi (Combination) ya somo hilo. Kwa sababu hiyo wanafunzi kushindwa kuchukua somo la michezo kwa vile hakuna Taasusi yake mara mwanafunzi anapofika “A” level.
Kwa sababu hiyo ameiomba Serikali iendeleze mchepuo wa somo hilo kutoka kidato cha Nne kuendelea hadi kidato cha sita na baadae muunganiko huo utaunganika na chuo kikukuu ambako somo hilo lipo.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa vitabu vya kufundishia somo la michezo (PE) na kuwafanya walimu wa michezo kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia uzoefu pekee. bajeti ndogo ya fedha zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya somo la michezo pamoja na upungufu wa walimu wa somo hilo ni moja ya changamoto pia zilizotajwa na Mkuu huyo wa shule.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Manyinga Mohamed Mbwiga amebainisha changamoto zinazokabili somo la michezo kuwa ni pamoja na ukosefu wa viwanja vya michezo, miundommbinu isiyorafiki kwa michezo mingi, kukosekana kwa kozi za mara kwa mara za somo la michezo na akamalizia kuiomba Serikali vifaa kwa ajili ya kufundishia somo la michezo ikiwemo Projector.
Shule teule za michezo ambazo Naibu Waziri Ulega alizitembelea Januari 28 ni pamoja na shule ya Msingi Manyinga na shule ya Sekondari ya Lusanga zilizoko wilayani Mvomero na shule ya Sekondari ya Morogoro katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na shule zote hizo zilipokea zawadi ya mipira kutoka kwa Naibu Waziri Ulega ikiwa ni ishara ya kuamsha chachu ya kupenda michezo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.