Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amelishauri Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) kuendeleza michezo mbalimbali katika makambi ya majeshi na sehemu za kazi ili kuibua vipaji vipya lakini bila kusahau kutekeleza jukumu lao la msingi la Ulinzi na Usalama.
Naibu Waziri Mwinjuma ametoa ushauri huo Septemba 15, 2024 wakati akifunga mashindano ya majeshi Tanzania yaliyozinduliwa Septemba 6, 2024 ambapo kwa mwaka huu mashindano hayo yamefanyika Mkoani Morogoro yakiwa na kaulimbiu inayosema "michezo ni furaha, Afya na ajira".
Amesema, kuna umuhimu mkubwa wa wanamichezo kutoka jeshini kushiriki michezo mbalimbali na kuweza kuliwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa hivyo ni jukumu lao kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo hao ili kuweza kufikia malengo.
"..Juhudi za kuendeleza michezo katika makambi na sehemu za kazi zizidi kuimarishwa na kuendelezwa.." Amesema Hamis Mwinjuma
kiongozi huyo ameendelea kutoa ushauri kwa Baraza hilo kuendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya michezo na mashirikisho ya vyama vya michezo nchini katika kuweka taratibu ambazo zitawezesha majeshi yetu kuendelea kutoa wawakilishi wengi wanaoliwakilisha Taifa katika mashindano ya Kimataifa.
Sanjari na hayo amelishauri Baraza hilo kuendelea kutoa mafunzo kwa walimu na waamuzi, kujenga viwanja vya michezo, na kuendeleza programu za kukuza na kuendeleza vipaji kwa vijana katika michezo ili kutengeneza wanamichezo watakaoshiriki mashindano mbalimbali.
Aidha, Naibu Waziri ameyataka majeshi yote kuendelea kutekeleza jukumu lao la msingi la kulinda watu na mali zao ili kuimarisha ulinzi na Usalama hapa nchini na taifa kuendelea kubaki kuwa kisiwa cha AMANI.
"Jambo la muhim kabisa, nichukue fursa hii kuwakumbusha utekelezaji wa jukumu lenu la msingi ambalo ni Ulinzi wa taifa letu na mipaka yake...." amesisitiza Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema michezo hiyo katika mkoa huo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa na wanamichezo wameonesha vipaji vyao huku akilishauri BAMMATA mwakani tena kuleta mashindano hayo mkoani Morogoro.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) Brigedia Jeneral Saidi Hamisi Saidi ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Michezo Taifa (BMT) kwa kuwezesha kutoa msaada wa kiufundi kwa BAMMATA huku akisema kumalizika kwa mashindano hayo ni muda wa kwenda kujipanga kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kitaifa na kimaifa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.