Mikoa yote hapa nchini kwa sasa ipo katika harakati za utoaji wa mafunzo ya mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma unaojulikana kama National e – Procurement system (NeST).
Mfumo wa NeST ni mbadala wa mfumo wa manunuzi ya Umma unaotumika sasa unaojulikana kama Tanzania National e Procurement System (TANePS) ulioanzishwa takribani miaka minne iliyopita.
Mfumo huu wa NeST ambao unaelezwa kuwa ni mfumo ulioundwa na wataalam wazawa wa Tanzania unaokuja kuwa mwarobaini wa kutatua changamoto kubwa ya uwepo wa milolongo mingi na iliyokuwa inachukua muda mrefu wakati wa manunuzi ya Umma hususani zabuni.
Changamoto hii ilitokana na mfumo wa TANePS ambao kwa namna moja au nyingine ulitoa mwanya kwa wadau wasio wazalendo wa utoaji na upokeaji wa rushwa, zabuni kutolewa kwa kufahamiana au kuwepo kwa upendeleo wakati wa michakato, hivyo kupelekea kuchelewesha mchakato wa manunuzi pamoja na gharama za bidhaa husika kuwa kubwa zaidi kuliko iliyoko sokoni.
washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa kielektroniki wa Manunuzi ya umma - National e - Procurement System (NeST) kutoka Halmashauri ya Ifakara wakiwa katika ukumbi wa mafunzo wakipewa mafunzo hayo. nyuma kabisa ni Mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Leopold Ngirwa akitoa usaidizi wa kitaalamu
Faida ya mfumo wa NeST ukiachia mbali kuundwa na wazawa wa ndani ya nchi yetu na kupelekea kuwepo kwa usiri na usalama wa nyaraka zetu za hapa nchini ukilinganisha na TANePS uliokuwa unamilikiwa na wageni, mfumo huo utaongeza uwajibikaji ndani ya mfumo na kutoa wigo mpana wa wadau katika kushiriki katika ununuzi, hapa ni pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Faida nyingine ni pamoja na kuharakisha michakato ya manunuzi na kupunguza matumizi ya nyaraka kwa kuwa na kazi kubwa za manunuzi zitazokuwa zinafanyika ndani ya mfumo na sio nje ya mfumo wa NeST, hivyo kuongeza thamani ya fedha yaani value for money kwa bidhaa husika.
Mafunzo hayo kwa sasa yanatolewa kwa ngazi ya Halmashauri kwa wataalamu sita (6) kutoka kila Halmashauri wakiwemo Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Vitengo vya Manunuzi, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa Mipango wa Halmashauri na wahasibu wa Halmashauri.
Awali, mafunzo ya mfumo wa NeST yalitolewa Jijini Dodoma kwa Wataalamu sita (6) wa kutoka kila Mkoa yaliyofanyika kuanzia Julai 31 hadi Agosti 4 mwaka huu ambayo yaliendeshwa chini ya Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wakishirikiana na Wataalamu mbalimbali kutoka PPRA na wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mimi kama Mtanzani, nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma hapa nchini (PPRA) kwa kuliona hilo na kubuni mbinu mpya ya kudhibiti fedha za Serikali ambazo ni kodi za wananchi zilizokuwa zinavuja kupitia eneo hili la manunuzi.
Sambamba na pongezi hizo kwa Serikali, kwa mujibu wa maelezo yanayotolewa kupitia mafunzo hayo ni kwamba mfumo wa TANePS utazimwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu na mfumo wa NeST utaanza kutumika rasmi kuanzia mwenzi Oktoba mosi mwaka huku kukiwa na angalizo kuwa taasisi yoyote itakayofanya manunuzi nje ya mfumo wa NeST baada ya mwezi Oktoba basi wahusika wake watachululiwa hatua kali za kinidhamu.
Wadau wanaunga mkono hatua hiyo ya Serikali na kwamba isisite kamwe kutekeleza maagizo yake ya kumchukulia hatua mkuu yoyote wa Taasisi ambaye hatatumia mfumo wa NeST, kwa kuwa kufanya hivyo Serikali itaokoa fedha nyingi zilizokuwa zinateketea bila sababu za msingi lakini pia kwa kutumia mfumo huu mpya itatoa fursa kwa wazabuni kupatikana kihalali.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.