Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Morogoro Dkt. Aifena Mramba amesema kwa sasa mfuko huo umesaidia kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wake wa sekta ya umma ukilinganisha na kabla ya kuazishwa kwa mfuko huo na kutoa rai kwa wanachama kutotoa kadi zao za Bima kutumiwa na watu wengine kwani amesema kufanya hivyo ni kinyume cha malengo ya mfuko na ni hujuma kwa mfuko huo.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Morogoro Dkt. Aifena Mramba akizungumza na watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Aifena ametoa rai hiyo Septemba 08 mwaka huu katika kikao chake na watumishi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo kikiwa na lengo la kutoa elimu ya Mfuko huo kwa watumishi hao.
Amesema, kumekuwa na utofauti mkubwa wa upatikanaji wa huduma ya Afya ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo mfuko huo haukuwepo namna watumishi wa umma walikuwa wanasumbuka katika kupata huduma ya Afya lakini kwa sasa wanachama wanapata matibabu ya uhakika katika hospitali zote za serikali na binafsi bila usumbufu wowote.
Katika hatua nyingine Dkt. Aifena amewatahadharisha wanachama wote wa mfuko wa NHIF ambao ndio wastaafu wa baadae kutogushi nyaraka wakati wa usajili wa mfuko huo au wakati wowote na kutotoa taarifa zisizo sahihi ili kuufanya mfuko huo kuwa hai na endelevu lakini pia kujiepusha na usumbufu wowote utakaoweza kujitokeza siku zijazo.
"... Mfuko huu umekuja kufeed hili gap la uchangiaji ambapo lilikuwepo, sasa tumeona improvement katika sekta ya Afya, tunafahamu wale watu wote wazima kama mimi hapa tunaokaribia kustaafu tunafahamu kabisa huko nyuma tulipotoka Hali ilikuwaje kabla ya mfuko huu kuwepo vituo vya serikali hata vituo vya private (binafsi)..." amesema.
Hata hivyo, Dkt. Aifena amewashauri watumishi hao kujiepusha na mtindo wa maisha wa sasa ambao una visababishi lukuki vikiwemo vyakula ambavyo baadhi ya vyakula hivyo vinasababisha magonjwa yasiyoambukizwa ambayo yanaongezeka kwa kasi na kuwa changamoto kwa watumishi wengi wa sekta ya umma ukiwemo ugonjwa wa shinikizo la damu.
Siyo hivyo tu bali Meneja huyo amewataka watumishi kujijengea utamaduni wa kufanya mazoezi kwani amesema asilimia kubwa ya wastaafu kutoka sekta ya umma wanakabiliwa na changamoto ya magonjwa hayo hivyo njia mojawapo ya kukabiliana nayo ni kufanya mazoezi.
Kwa upande wao watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Herman Tesha kwa niaba yao ameahidi kuwa mabalozi wazuri wa mfuko huo na kusimamia ipasavyo pamoja na kuwa makini na viambatanisho vya mfuko huo wakati wa kusajili ili kupata wanachama walio halali.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawla na Rasilimali watu Bw. Herman Tesha akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Sambamba na ahadi hiyo Bw. Tesha amewaasa watumishi hao kuepuka kutoa taarifa za udanganyifu wakati wa usajili kwani ni ukiukwaji maadili na kwamba atakayebainika kufanya udanganyifu huo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Naye, Afisa wanachama wa NHIF Mkoa wa Morogoro Bw. Hema Samson Daniel amesema, mfuko huo una wachangiaji wasiozidi Milioni 2 lakini una watumiaji zaidi ya Milioni 20, hii inatokana na watumishi wasio waadilifu kuruhusu watu wengine kupata matibabu au huduma za Afya kupitia kadi zao za Bima hiyo jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ukitoa huduma hiyo kwa makundi ya watumishi wa umma, wafanyakazi wa sekta binafsi na wanachama binafsi.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.