Kocha wa timu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mpira wa kikapu upande wa wanaume Bw. Alfred Ngalaliji, amesema NIDHAMU na UTULIVU uwanjani vimefanya timu yao kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao timu ya Polisi kwa kuwachapa magoli 57 kwa 45 na hivyo kuwa washindi kwenye mchezo huo wa kwanza kwao.
Bw. Ngalaliji amebainisha hayo Septemba 7, 2024 wakati wa mechi yao ya kwanza ya mashindano ya michezo ya majeshi nchini, kwenye mechi yao ya mchezo wa mpira wa kikapu uliofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoinne (SUA) kilichopo mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, kocha huyo amesema, Mchezo kati yao na Polisi ulikuwa mgumu hatua za awali lakini baada ya kusoma mchezo huo vizuri pamoja na mbinu zao walilazimika kubadilisha mbinu na kufanikiwa kuwamudu na kuibuka washindi kwenye mchezo huo.
"..kama kawaida yetu nidhamu ndiyo imetufanya tufanye vizuri kwenye mchezo huu, na tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi kwenye mashindano haya ya BAMMATA kwa upande wa Mpira wa Kikapu na ubingwa lazima uchukuliwe na JKT.." amesema Afred Ngalaliji.
Aidha, amesema wataendelea na kichapo kwa yoyote atakayekuja mbele yao kwa sababu wanatimu nzuri ambapo amebainisha kuwa matarajio ni kuchukua ubingwa kwenye michezo mbalimbali huku akitamba kuwa wamezoea kuishi kwenye nafasi ya kwanza, na kuwatahadharisha wapinzani wao kuwa waangalie nafasi ya pili au nafasi nyingine lakini nafasi ya kwanza ni ya JKT.
Michezo ambayo mpaka sasa JKT imeshinda ni pamoja na mchezo wa Mpira wa Kikapu (Basketball) upande wa wananume, mchezo wa Mpira wa Mikono wa wanawake (Handball).
ambapo katika mchezo wa mpira wa mikono JKT iliibuka na ushindi wa magoli 47 dhidi ya Magereza iliyoambulia magoli 7 pekee.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.