Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu hapa nchini (NIMR) imeanza utafiti wa kufuatilia ugonjwa wa Malaria kwa kutumia mbinu za vinasaba kwa lengo la kuchunguza mabadiliko ya vimelea vya Malaria ili kubaini mbinu mpya zitakazotumika kupambana na kutokomeza ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa wakati wa warsha ya wadau wa utafiti wa kutumia mbinu za vinasaba katika ufuatiliaji wa ugonjwa Malaria nchini Tanzania iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo Mkurugenzi wa Kuratibu na kukuza Utafiti hapa nchini (NIMR) Dkt. Paul Kazyoba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NIMR amesema katika kufanya tafiti za ugonjwa wa Malari NIMR imeshirikiana na Mpango wa Taifa wa kuthibiti Malaria na kufanikisha tafiti nyingi huko nyuma.
Dkt. Kazyoba amebainisha kuwa NIMR kwa kushirikiana na NMCP wamefanikiwa kupata ufadhiri wa kufanya utafiti na kujenga uwezo wa kutumia mbinu za vinasaba katika kufuatilia ugonjwa wa malaria na utafiti huo utafanyika kwa miaka mitatu na nusu na kuhusisha mikoa 13 ya Tanzania bara na kwamba fedha na watendaji wanahitajika kufanikisha hilo.
“Katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inatekeleza mpango mkakati wenye lengo la kutokomeza malaria ifikapo 2030, tunahitaji kuongeza nguvu ikiwemo rasilimali fedha na watendaji katika mapambano dhidi ya malaria” alisema .
Akifungua Warsha hiyo ya siku moja Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameishauri Wizara ya Afya na Taasisi husika zote kuzipitia ripoti zote za mapendekezo yatakayotolewa kupitia utafiti huo ili kuyafanyia kazi ikiwemo kutumia taarifa na matokeo ya utafiti katika kufanya maamuzi na kutunga sera za kutokomeza ugonjwa wa Malaria hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora amesema ugonjwa wa Malaria katika Mkoa huo ambao kwa sasa ni wa kwanza kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
Naye, Naibu Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria – NIMC Dkt. Samweli Lazaro ambaye ameiwakilisha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema utafiti huo umeanza Mei mwaka jana na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu hadi Octoba 2023.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Dkt. Simon Chacha amesema Mkoa wa Kigoma unashika nafasi ya pili Kitaifa kwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria hata hivyo, jitihada za kuutokomeza ugonjwa huo zimeendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kupulizia dawa ya kuua mbu majumbani na kwenye mazalia yake.
Katika hatua nyingine Dkt. Chacha ametoa wito kwa watanzania kutumia Elimu ya Afya inayotolewa kujikinga na maambukizi ya mbu lakini pia kufika katika vituo vya Afya mapema endapo wanahisi dalili za Malalia ili kupima na kupewa huduma za matibabu.
NIMR ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya ambayo ilianzishwa na sheria ya Bunge Na. 23 ya mwaka 1979 (Cap. 59, R.E. 2002) na kuanza kazi rasmi Oktoba 1980 baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.