Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Morogoro kwa kupanua wigo wa utoaji huduma hapa nchini kwa kuwafikia wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, wachimbaji wadogo na wasanii katika Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akiongea na Viongozi, Waajiri, wafanyakazi na wanachama wa mfuko wa NSSF Morogoro kwenye ufunguzi wa kongamano la waajiri Mkoani Morogoro.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa pongezi hizo Disemba 16 mwaka huu wakati akifungua kongamano la Waajiri katika Mkoa wa Morogoro lililowakutanisha waajiri kutoka Mashirika, na Taasisi mbalimbali katika Mkoa huo.
kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF uliopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Fatma Mwassa akipokea zawadi kutoka kwa viongozi wa mfuko wa NSSF baada ya ufunguzi wa kongamano la waajiri Mkoani Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema NSSF katika Mkoa huo imehakikisha kuwa waajiri wanatekeleza wajibu wao wa msingi wa kuwasilisha michango ya waajiriwa wao kwa wakati hivyo kuepusha migogoro na waajiriwa wao.
“... NSSF imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha waajiri wanatekeleza jukumu lao la msingi la kuwasilisha michango kwa wakati lakini pia ninaziona juhudi kubwa za NSSF Morogoro katika kuhakikisha makundi mbalimbali ya sekta isiyorasmi yanaandikishwa, hongereni sana wananssf Morogoro kwa kazi nzuri..” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa sasa watanzania wanaziona juhudi za shirika hilo kwa sababu sehemu kubwa ya makusanyo ya fedha zinatumika kutekeleza miradi mikubwa ambayo inaikuza NSSF kama shirika na watanzania wote.
Sambamba na hilo, Mhe. Fatma mwassa ametumia kongamano hilo kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kusimamia sekta ya hifadhi za jamii hapa nchini, na kuridhia kanuni mpya ya kikokotoo ambacho kimenufaisha kundi kubwa la wananchama wa NSSF.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewasisitiza waajiri katika Mkoa huo kuendelea kutekeleza wajibu wao wa msingi wa kuwaandikisha wafanyakazi wao katika mfuko wa NSSF pamoja na kuwasilisha michango yao stahiki kwa wakati.
Awali Meneja wa NSSF Mkoa wa Morogoro Bi. Amina Kassim wakati akitoa tathimini ya utendaji wa kazi wa NSSF katika Mkoa huo amesema kazi kubwa ya NSSF Morogoro ni kuwaandikisha waajiri na wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa wanachama wake.
Meneja wa Mfuko wa NSSF Mkoani Morogoro Bi. Amina Kassim akitoa tathmini ya utendaji wa NSSF Morogoro kwenye ufunguzi wa Kongamano la waajiri Mkoa wa Morogoro.
Amesema NSSF Morogoro inakusanya kiasi cha shilingi Bilioni sita kwa mwezi na kulipa mafao Bilioni Moja nukta Moja kwa mwezi, ameongeza kuwa Mfuko huo unawanachama 338,000 na wastaafu hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu 2022 walikuwa 1,269.
Aidha, Bi. Amina Kassim ametaja miradi ambayo NSSF katika Mkoa huo inamiliki ikiwemo Mradi wa Kiwanda cha Sukari cha Mkurazi kilichopo Wilayani Kilosa, ambapo kinatarajia kuanza uzalishaji mwezi Machi 2023, pia inajengo la Mafao ambalo ni kitega uchumi cha NSSF pamoja na ofisi za kupangisha ambazo baadhi ya taasisi za kibenki zimekodi.
Pamoja na mafanikio hayo Meneja huyo amesema kunachangamoto ambazo wanakutana nazo zikwemo za waajiri kuchelewa kupeleka taarifa za wanachama wao kwa wakati, waajiri kutowasajiri wafanyakazi wao katika Mfuko, waajiri kushindwa kutoa mikataba kwa wafanyakazi wao.
Kwa upande wake Bw. James Oigo Meneja Usimamizi wa Mafao kutoka Makao makuu ya NSSF amesema kupitia makongamano hayo yanawezesha kuwafikia wafanyakazi wengi zaidi, na lengo la makongamano hayo ni kutoa elimu, kukumbushana wajibu wa wanachama na waajiri pamoja na kupokea mrejesho kutoka kwa wanachama wao.
Meneja Usimamizi wa Mafao ya Mfuko wa NSSF Bw. James Oigo akiongea na waajiri, viongozi na wanachama wa mfuko huo.
Kongamano hilo lina lengo la kutoa elimu ya hifadhi za jamii kwa waajiri, kutoa elimu ya mabadiliko ya kisheria ya hifadhi za jamii kama ile ya kikokotoo, kuwakumbusha waajiri kupeleka michango ya wafanyakazi katika mfuko, na kutoa elimu ya matumizi ya Tehama katika kukusanya na kuhifadhi taarifa za waajiri na wafanyakazi katika mfumo wa kielektroniki.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akitoa zawadi kwa waajiri wa Mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria katika mfuko huo wa NSSF.
Baadhi ya picha za Mhe. Fatma Mwassa akiwa kwenye picha pamoja na waajiri, viongozi, wafanyakazi na wanachama wa NSSF Mkoa wa Morogoro baada ya ufunguzi wa kongamano la waajiri Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.